MRADI wa maji Nangombo -Kilosa wilayani Nyasa mkoani Ruvuma unaotekelezwa kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni nne unatarajia kuwanufaisha wananchi wapatao 13,323 utakapokamilika.
Hayo yamesemwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed .
Amesema mradi huo unatarajia kuvinufaisha vijiji vya Nangombo,Likwilu,Ruhekei na Kilosa vilivyopo katika mji wa Mbambabay na kwamba uwezo wa chanzo cha maji unalenga pia kufikisha huduma ya maji eneo la Mbambabay.
“Mradi utasaidia kupunguza magonjwa ya milipuko kwa jamii kutokana na kuimairika kwa huduma ya maji,jamii itapata muda wa kufanya shughuli za maendeleo’’,alisema.
Hata hivyo amesema mradi huo wa miezi sita ulitakiwa kukamilika Juni 18,2023 na kwamba utekelezaji wa mradi huo bado haujakamilika kwa wakati kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa msamaha wa kodi,malipo ya awali na kasi ndogo ya Mkandarasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri amesema ,hivi sasa utekelezaji wa mradi umesimama kutokana na kuisha kwa muda wa mkataba wa Mkandarasi ambapo,serikali imemua kutekeleza mradi huo kwa kutumia wataalam wa ndani.
Amesema hivi sasa taratibu za kusitisha mkataba na Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi zinaendelea na kwamba matarajio ni kwamba kazi hiyo inatarajia kutekelezwa kwa miezi nane kuanzia Juni 2024.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Ahmed Abbas amesisitiza utekelezaji wa mradi huo,kufanywa na wataalam wa ndani kwa uadilifu kwa sababu mradi umechelewa.
Amesema wananchi wanatamani kupata huduma ya maji kwa kuwa serikali imetoa mabilioni ya fedha kuhakikisha mradi huo unakamilika hivyo amewataka RUWASA kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kutekeleza mradi huo.
Baadhi ya wananchi mjini Mbambabay wameishukuru serikali kwa kutoa fedha za mradi huo ambao wamesema ukikamilika utakuwa msaada mkubwa kwa jamii kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.