Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, ameendelea na ziara yake katika Kata ya Kilagano, wilayani Songea Vijijini. Ziara hiyo imelenga kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Mgazini na Lugagala, ambapo amewapongeza kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi wa vitongoji vyote kumi na mbili. Amesema ushindi huo ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wananchi kwa chama hicho na uongozi wake.
Katika mkutano wake na wananchi, Mwenyekiti Oddo Mwisho ametoa fursa ya maswali kuhusu changamoto zinazowakabili. Moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni mgogoro wa Mlima wa Lihanje, ambao wananchi wa vijiji hivyo wameiomba serikali kuutatua haraka. Wananchi wamelalamika kuwa mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu bila suluhisho, hali inayokwamisha maendeleo yao.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa ameeleza kuwa serikali inatambua changamoto hiyo na inafanya jitihada kuhakikisha suluhisho la kudumu linapatikana. Amewahimiza wananchi kuwa na subira huku serikali ikishughulikia suala hilo kwa kufuata taratibu na sheria. Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa serikali wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa ilani ya CCM ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika ziara hiyo, Oddo Mwisho amegusia changamoto nyingine zinazowakabili wananchi wa Kata ya Kilagano, ikiwemo ukosefu wa umeme katika Shule ya Sekondari Mtopesi. Amesema serikali ina wajibu wa kuboresha miundombinu muhimu kama umeme, maji, barabara, afya na elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini. Pia, amepongeza uteuzi wa Dkt. Emanuel Nchimbi na Dkt. Hassan Mwinyi kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM. Amesema uteuzi wa Dkt. Nchimbi ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Ruvuma, hivyo wananchi wanapaswa kujivunia na kuendelea kumuunga mkono.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.