Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Mhandisi Marryprisca Mahundi amefanya ziara ya katika vijiji nane vilivyopo katika Kata nne za Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma kwa lengo la kusikiliza Kero za mawasiliano zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Vijiji hivyo ni Igawisenga,Wino,Maweso,Matetereka,Mkongotema,Lutukira,Ndelenyuma na Mbangamawe ambapo vijiji hivyo vipo katika kata za Wino,Matetereka,Mkongotema na Gumbiro.
Ziara hiyo ya Naibu waziri imelenga kusikiliza changamoto za wananchi wa Madaba hususani zinazohusu sekta ya mawasiliano ili kuweza kuzitatua kwani wananchi hao wamekuwa wakisumbuliwa na uwepo wa mawasiliano hafifu mara kwa mara hali inayokwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuathiri huduma nyingine za kijamii.
Amesema Wizara ya Habari inakusudia kufungua kituo cha redio Jamii katika Halmashauri ya Madaba ili wananchi waweze kuitumia redio hiyo katika shughuli mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mdaba na kupata taarifa za kitaifa na kimataifa kwa urahisi kwa kuunganishwa na redio hiyo.
Katika ziara hiyo Naibu waziri amebainisha juhudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha maeneo ya pembezoni na nchi nzima zinaimarika katika sekta ya mawasiliano ili kuweza kwenda sambamba na uchumi wa kidijitali na mabadiliko ya teknolojia
"Namna ambavyo mnapata mawasiliano ya kusuasua, haimfurahishi Mheshimiwa Rais ametutuma kutoka wizarani tuhakikishe tunapita, tunajionea, tunaongea na nyie mwisho wa siku tunakuja kuimarisha mfumo wa mawasiliano" ameeleza
Naye Mhandisi Shirikisho Mpunji kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) amesema walitarajia kuwa mnara uliopo eneo la Lilondo kata ya Madaba ungewezesha Mawasiliano maeneo ya vijiji vya Madaba lakini hali ya kijiografia imeathiri uwezekano huo na hivyo maeneo hayo yanahitaji minara mingine
Amebainisha kuwa Wizara imeandaa mradi kwa ajili ya kujenga minara 636 nchini ambapo kati ya minara hiyo, mitano itajengwa katika kata tano za Halmashauri ya Madaba ili kutatua changamoto za mawasiliano zinazowakabili wananchi katika maeneo hayo
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imelenga Kuwezesha utoaji wa huduma za uhakika na za gharama nafuu za Habari, Teknolojia ya Habari, Mawasiliano ya simu na Posta kwa kuweka mazingira yanayokuza ubunifu katika kuibadilisha Tanzania kuwa na Uchumi wa Kidigitali
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.