BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 12 katika shule tatu za msingi zilizopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akikabidhi vifaa hivyo katika shule hizo,Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amezitaja shule zilizopata vifaa hivyo kuwa ni shule ya msingi Legele iliyopata mabati 60 kwa ajili ya kuezeka darasa la kwanza na choo.
Shule nyingine ni Mshanganokati iliyopewa madawati 80 na shule ya msingi Chandamali ambayo imepewa meza 21,viti 21 na kabati nne ambapo amesisitiza kuwa Benki ya NMB imeamua kushirikiana na jamii kwa kutoa msaada katika shule hizo tatu .
“Ingawa Benki ya NMB inapokea maombi mengi,naweza kuahidi kwamba tutaendelea kutoa misaada hii kadri ambavyo tutakuwa tunaweza,tumejipanga kutoa huduma bora kwa jamii’’,alisisitiza Shango.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Tawi la Songea David Zake akizungumza kwa nyakati tofauti katika zoezi la utoaji vifaa hivyo,amesema Benki ya NMB ni sikivu kwa sababu imekuwa inarudisha mapato yake ya asilimia moja kwa jamii kila mwaka .
Amesema hali hiyo ndiyo iliyosababisha shule hizo tatu kuwa miongoni mwa shule ambazo zimepata mchango mkubwa kutoka NMB.
Mgeni rasmi katika hafla ya utoaji msaada huo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Songea Pendo Ndumbaro amesema NMB imemaliza chagamoto ya madawati iliyokuwa inaikabili shule ya msingi Mshanganokati ambayo ilisababisha baadhi ya watoto kukaa chini kwa kukosa madawati.
Amesema NMB imekuwa karibu kwa jamii wilayani Songea kwa kutoa misaada mbalimbali katika shule na vituo vya afya ambapo amesisitiza kwa kazi zinazofanywa na Benki hiyo zinaunga mkono jitihada za serikali kusaidia wananchi.
Naye Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Songea Zakia Fandey amesema msaada huo utaongeza mahudhurio mazuri ya wanafunzi hasa katika shule msingi Mshanganokati iliyokuwa na uhaba mkubwa wa madawati na kwamba ufundishaji na ujifunzaji utaimarika .
Rehema Milinga ni Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mshanganokati ameishukuru NMB kwa msaada wa madawati ambapo amesema watoto walikuwa wanaandika chini kwa kuegemea kwenye ukuta ambapo hivi sasa asilimia kubwa ya watoto wanakaa kwenye madawati.
Nao wanafunzi Mary Haule na Happy Mbunga kwa niaba ya wanafunzi wenzao wameishukuru NMB kwa msaada wa madawati na mabati vifaa ambavyo wamesema vitawawezesha kusoma kwenye mazingira mazuri.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 12,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.