Oparesheni ya kuwaondoa wafugaji katika maeneo wasiostahili kuanza mkoani Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameagiza wafugaji wote ambao wameingiza mifugo yao kwenye maeneo wasiostahili warudi kwenye maeneo yao ya vitalu.
Ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara wakati anasuluhisha mgogoro wa wakulima na wafugaji wa Kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo uliosababisha watu wanne kupoteza Maisha.
Mkuu wa Mkoa ameagiza wafugaji wote waliongiza mifugo yao bila vibali,wapeleke mifugo yao katika maeneo yenye vitalu vya wafugaji ambapo katika Mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru ina vitalu vya kutosha kwa ajili ya wafugaji.
“Mkoa wa Ruvuma ndiyo Mkoa pekee nchini ambao umetenga vitalu kwa ajili ya wafugaji,Katika wilaya ya Tunduru kitalu kimoja kina hekari 500,hadi sasa kuna vitalu 107 ambavyo vipo wazi kwa ajili ya wafugaji’’,alisisitiza.
RC Thomas ametoa mwezi mmoja kwa wakuu wa wilaya zote kusimamia zoezi la utambuzi wa mifugo yote iliyopo kwenye maeneo yao kama ina vibali na namna vibali vilivyotolewa.
“Utoaji wa vibali vya mifugo hivi sasa umekuwa ni holela na kuna mazingira ya rushwa,kila mtu amekuwa anatoa vibali hali inayosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji’’,alisema Kanali Thomas.
Hata hivyo amesema kuanzia Novemba 10,2022 ni marufuku kuingiza mifugo mkoani Ruvuma hadi hapo uhakiki wa kubaini mifugo utakapokamilika.
Amesisitiza kuwa zoezi la utambuzi wa mifugo linaanza Novemba 10 na linatarajia kukamilika Desemba 9 mwaka huu na kwamba baada ya hapo oparesheni kabambe ya kuondoa mifugo iliyopo katika maeneo yasiyostahili itafanyika katika Mkoa mzima.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua za kinidhamu wenyeviti wote wa vijiji na watendaji wanaohusika katika kuleta migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU kuchunguza tuhuma dhidi ya wenyeviti wa vijiji ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji.
Kwa upande wake Awadhi Haji Kamishina wa Operasheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania akizungumza kwenye mkutano huo,amesema migogoro ya wakulima na wafugaji hivi sasa imeshamiri katika Kanda ya Kusini.
Amesema migogoro hiyo inasababishwa na watu wachache waliopewa dhamana kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo rushwa hivyo kuruhusu wafugaji kuingia katika maeneo ambayo hawastahili.
Amewataka wafugaji walioingia kinyume na taratibu kuondoka na kwamba vitendo hivyo havitavumiliwa na matukio hayo yakijitokeza tena jeshi la polisi litachukua hatua kali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu amesema serikali hairidhiki na mifugo inayoingia kwenye mashamba ya wakulima na imekuwa inachukua hatua kukabiliana na hali hiyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 12,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.