Mji wa Peramiho uliopo Wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa miji ya zamani yenye historia ya kipekee katika ukanda ya kusini.
Mji wa huo unafahamika zaidi nje ya nchi pengine kuliko miji mingine iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo kuwa na historia ya namna yake kipekee ikiunganisha Tanzania na mataifa ya Ulaya.
Historia ya mji wa Peramiho uliopo kilometa 24 tu kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma Songea inaunganishwa na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini Ujerumani,ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
Wabeneditine hao waliingia kwa mara ya kwanza katika mji huo mkongwe mwaka 1898 wakiongozwa na Kasian Spiss.Tangu wakati huo wabenediktine hao wamekuwa wakifanya mambo yanayoutangaza mji huo hali iliyosababisha kuutambua mji wa Peramiho kuwa ni mji unaokidhi vigezo kuwa mji wenye utalii wa kiutamaduni.
Kanisa la pili la Peramiho lina saa ya maajabu ambayo ilitengenezwa kwa vyuma zaidi ya miaka 70 iliyopita na wajerumani na kwamba tangu mwaka 1946 ilipotengenezwa hadi sasa saa hiyo haijawahi kusimama wala kupoteza majira jambo ambalo linawashangaza na kuwavutia wengi kutembelea kanisa hilo ili kuiona saa hiyo ya maajabu.
Kanisa kuu la Peramiho lililitumia matofali zaidi ya milioni tatu,ujenzi ulianza wakati Askofu Gallus Steiger na bruda Gisral Stumpf ambaye aliandaa mchoro wa kanisa hilo mwaka 1940 na mwaka 1941 msanii wa majengo Hans Burkard wa Uswis alisanifisha rasimu ya michoro hiyo na kumrejeshea Askofu Gallus mwaka 1943 na michoro kukamilishwa na bruda Gislar.
Kazi ya ujenzi wa kanisa hilo ilianza Julai 6,1943 na kumalizika Septemba 9,1943.Kenchi za mihimili ya kanisa kuu hilo zenye uzito wa tani tano chini ya usimamizi wa mabruda Nonosius Bleicher na Menas Leicht ilifanyika na kupandishwa kwa mashine maalum iliyotengenezwa na bruda Jucundus Weigele Agosti 1946.
Mnamo Novemba 24,1945 vigae vyote 120,000 vilikuwa tayari kwa ajili ya kuezekea kanisa hilo na mnamo mwaka 1948 kanisa kuu Peramiho lilibarikiwa na padre Heribert na padre Gerod Rupper akawa padre wa kwanza kuhubiri katika kanisa hilo jipya.
Makala hii Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.