Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Ujenzi kukamilisha maandalizi na kuanza kujenga upya barabara ya Songea - Njombe - Makambako (km 295) pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko ya Songea (Songea Bypass) yenye urefu wa kilometa 16 kwa kiwango cha lami.
Rais Samia ametoa agizo hilo kwa Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake ya kikazi uliofanyika katika Uwanja wa Majimaji Songea Mkoani humo.
“Ninafahamu barabara ya Songea - Njombe hadi Makambako sasa inahitaji matengenezo makubwa tayari nimeshaielekeza Wizara ya Ujenzi kuishughulikia pamoja na barabara ya mzunguko ya bypass ya hapa Songea hatua za kuanza kuijenga zipo mwishoni”, amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Samia ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2024 Serikali itakuwa imempata Mkandarasi kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi wa barabara ya Lukuyufusi - Mkenda (km 60) kwa kiwango cha lami ili kuweza kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na nchi jirani ya Msumbiji.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amesema kuwa tayari ameidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 3.5 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara ya Amani Makoro hadi Luanda (km 35) kwa kiwango cha lami ambapo tayari Serikali imekamilisha sehemu ya barabara hiyo kilometa tano kuanzia Kitahi hadi Makolo.
Rais Dkt. Samia amewaeleza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuwa Serikali ina mpango wa kuunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80.
Rais Dkt. Samia akiwa Mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi, Katika Sekta ya Ujenzi alikagua ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea ambao umekamilika kwa asilimia 100 na kugharimu shilingi Bilioni 40.87 pamoja na kufungua barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na kugharimu Shilingi Bilioni 122.76
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.