Na Albano Midelo,Songea
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Angela Kairuki amesema serikali imeanza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuandaa mpango wa majadiliano na serikali ya Ujerumani kuona namna bora ya kurejesha malikale za Ruvuma na maeneo mengine nchini.
Hayo yamesemwa katika hotuba ya Waziri Kairuki iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwenye kilele cha kumbikizi ya miaka 119 ya mashujaa 67 wa vita ya Majimaji waliouawa kwa kunyongwa na wajerumani Februari 27,1906 mjini Songea.
Moja ya malikale zilizochukuliwa na wajerumani ni kichwa cha Jemedari wa Wangoni Nduna Songea Mbano ambaye alipigwa risasi na wajerumani kisha kukata kichwa chake na Kwenda kukihifadhi nchini Ujerumani.
Baraza la Wazee wa Makumbusho ya Majimaji kwa muda mrefu wamekuwa wanaidai serikali ya Ujerumani kuwarejeshea fuvu la Songea Mbano ambaye alionesha upinzani mkali kwa wajerumani katika harakati za kupinga ukoloni.
Waziri Kairuki amesema serikali imekusudia kuona watanzania wananufaika na malikale zilizochukuliwa na wakoloni wa kijerumani ili watanzania waweze kunufaika na malikale hizo zilizopo nchini Ujerumani.
Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amesema historia ya harakati za ukombozi wa Tanzania bara haiwezi kuandikwa bila kuwataja mashujaa wa vita ya Majimaji ambao walikubali kupoteza Maisha yao ili kutetea Taifa lao.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania Mistica Ngongi amesema kumbukumbu za mashujaa wa vita ya Majimaji zitawezesha kizazi cha sasa na kijacho kuona na kujifunza namna babu zetu walivyoyatoa Maisha yao katika kupigania Uhuru.
Amesisitiza kuwa Vita ya Majimaji inawakumbusha tunu za babu zetu ikiwemo ya uzalendo, ujasiri, uthubutu na umoja wao katika kutetea maslahi ya nchi dhidi ya ukoloni.
Akizungumzia kuhusu masalia ya watu waliouawa katika Vita ya Majimaji likiwemo fuvu la Jemedari wa wangoni Nduna Songea Mbano,Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt.Frank Walter Steinmeier,akizungumza baada ya kuwafariji wahanga mjini Songea, alisema masalia hayo kutoka Afrika Mashariki yalisafirishwa hadi nchini Ujerumani na kuhifadhiwa katika makumbusho na hifadhi za kiatropolojia ambako kuna maelfu ya mafuvu ya vichwa vya binadamu.
Alisema serikali ya Ujerumani inaendelea na jitihada za kutafuta fuvu la kichwa cha shujaa Songea Mbano nchini Ujerumani ambapo ameitaja changamoto kubwa iliyopo ni kupima na kutambua masalia halisi ya binadamu kwa fuvu la mlengwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.