WAKALA wa barabara za vijijini na mijini Tanzania(TARURA) umesema,ujenzi wa daraja katika mto Makomba kata ya Langiro wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limekamilika kwa asilimia 100.
Meneja wa TARURA wilaya ya Mbinga Oscar Mussa ambapo ameeleza kuwa,daraja hilo limegharimu shilingi milioni 95 na sasa lipo kwenye muda wa matazamio ya mwaka mmoja unaomalizika mwezi Machi mwaka huu.
Mussa alisema,kukamilika kwa daraja hilo linalounganisha vijiji vinne vya Mkoha na Mkoha Asili kwa upande mmoja na kijiji cha Langiro na Langiro-Asili kunatoa fursa kwa wananchi wa maeneo hayo kusafirisha mazao hasa zao maarufu la kahawa linalozalishwa kwa wingi katika vijiji hivyo.
Alisema,daraja hil ni muhimu sana kwa kuwa,wananchi wa kata ya Langiro wanategemea kupata huduma za afya na huduma nyingine za kijamii kata jirani ya Maguu,kwa hiyo litawasaidia wananchi kupata huduma hizo kwa wakati.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Tarura inatarajia kujenga daraja lingine lenye urefu wa mita 10 katika kijiji cha Mkoha asili mpakani mwa wilaya ya Mbinga na Nyasa ikiwa ni mwendelezo wa mpango wake wa kuunganisha maeneo mbalimbali hapa nchini kwa barabara.
Amewataka wananchi kuwa na uchungu wa kodi zao,kwa kutunza na kulinda barabara na kutofanya shughuli zozote kando kando ya barabara zinazoendelea kujengwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na zitumike kama chachu ya kuwaletea maendeleo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita,kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kiunganishi muhimu kwa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Mbinga.
John Komba mkazi wa kijiji cha Mkoha alisema,walikuwa wakiteseka sana wanapohitaji kusafirisha mazao na bidhaa nyingine na hata wanapotaka kufuata huduma za kijamii zikiwemo za afya zinazopatikana kijiji jirani cha Maguu na katika kituo cha Afya Mapera.
Alisema,walikuwa na maisha magumu zaidi hasa wakati wa masika kwani wananchi waliotaka kwenda upande wa pili kutoka kijiji cha Mkoha na Mkoha asili walilazimika kusubiri kati ya masaa manne hadi sita ili maji ya mto huo yapungue.
Alisema,hali hiyo ilisababisha kupoteza muda mwingi ambao wangeweza kutumia katika shughuli zao za uzalishaji mali na maendeleo kwa ujumla.
Mkazi wa kijiji cha Langiro Martin Kapinga alisema,kabla ya kujengwa kwa daraja hilo,mto Makomba ulikuwa kikwazo kikubwa kwao kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi sita.
Kapinga,amewapongeza wataalam wa Tarura kwa kusimamia mradi huo na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga.
Joseph Kinunda mkazi wa kijiji cha Mkoha alisema kabla ya kujengwa kwa daraja,walikuwa kwenye mateso makubwa pindi wanapohitaji kuvuka kwenda maeneo mengine na kueleza kuwa, baadhi ya wananchi wenzao wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji walipojaribu kuvuka katika mto huo.“sisi wananchi wa maeneo haya tunaishukuru sana serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt Samia Hassan,kwani katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wake tumeshuhudia mambo mengi mazuri yanafanyika ikiwamo ujenzi wa daraja hili”alisema Kinunda.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.