Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali muhimu kama elimu, afya, maji, barabara, nishati, kilimo, na miundombinu mingine ikiwemo bandari.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Ushauri Mkoa RCC amesema Ili kufanikisha malengo ya miradi hii, wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa utekelezaji wake ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Kanali Abbas amesema Mkoa wa Ruvuma umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa mujibu wa Kanali Abbas Kwa mwaka wa fedha 2023/24, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 20.33, sawa na asilimia 117 ya lengo la shilingi bilioni 17.43.
Aidha, halmashauri za mkoa huo zimekusanya jumla ya shilingi bilioni 31.46, ikilinganishwa na lengo la bilioni 27.88, ikiwa ni asilimia 112.85 ya makadirio ya makusanyo.
Kutokana na mafanikio hayo, uongozi wa mkoa umepongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi na wataalamu wa halmashauri, wakiongozwa na wenyeviti wa halmashauri kwa juhudi zao katika kuhakikisha makusanyo ya mapato yanaimarika.
Nayo wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma wamepongezwa kwa kulipa kodi kwa hiari, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato ya serikali.
Mapato haya yanaiwezesha serikali kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.