MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ametoa zawadi ya Sh200,000 kwa walimu wa shule ya Sekondari London Manispaa ya Songea kufuatia shule hiyo kufanya vizuri katika mitahani ya kidato cha sita kwa miaka miwili mfululizo.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba yake,Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Mashauri Ndaki alisema, Mkuu wa mkoa amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na walimu wa shule hiyo ambazo zimewezesha kushika nafasi ya kwanza kimkoa.
Aidha alisema, hata katika matokeo ya mtihani ya kitaifa shule ya Sekondari Londoni imekuwa miongoni mwa shule ambazo zimeshika nafasi za juu katika matokeo ya mitihani ya kitaifa na hivyo kuutangaza vyema mkoa huo.
Alisema, Mkuu wa mkoa amefurahishwa na ufaulu wa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2020 ambapo zaidi ya wanafunzi 65 walichaguliwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu.
Aidha alisema, Mkuu wa mkoa ameridhishwa namna uongozi wa shule hiyo ulivyosimamia vizuri ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwa ya kwanza katika kutekeleza miradi ya Covid-19 katika Manispaa ya Songea kupitia fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid -19.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ibuge,ametoa mifuko ya saruji 150 kwa shule ya msingi Sabasaba kata ya Matarawe kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa.Afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Emmanuel Kisongo,amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani humo,kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ili waweze kufanya vizuri katika masomo.
Alisema,suala la kuchangia chakula ni wajibu wa wazazi na walezi kwa sababu mtoto hasipopata chakula itakuwa vigumu kuelewa kile anachofundishwa na walimu na hivyo kufanya vibaya katika masomo na mitihani.
Amewataka wazazi na walezi kutoelewa vibaya suala la elimu bure, kwani Serikali ina wajibu wake na wao kama wazazi wana wajibu na majukumu ya kuwapatia watoto wao mahitaji yote muhimu ikiwemo chakula,sale na vifaa vya masomo.
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, ambapo ujenzi wa madarasa hayo utawezesha watoto wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwakani kupata nafasi katika shule watakazopangiwa.
Pia Kisongo, amempongeza Rais Samia kwa kumteua Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kwani kwa muda mfupi tangu alipofika mkoani humo Brigedia Jenerali Ibuge amekuwa mstari wa mbele kusimamia suala la elimu na hivyo kuwezesha mkoa huo kufanya vizuri kitaaluma.
Alisema, Jenerali Ibuge ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine kwani amesaidia sana kuinua sekta ya elimu kwa kutoa zawadi na motisha kwa walimu na shule mbalimbali zilizofaulisha vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari London Ester Kulumla, amemshukuru Mkuu wa mkoa kwa kutambua juhudi za walimu wa shule hiyo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata kile wanachostahili na wanafanya vizuri katika masomo yao.
Alisema, katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita mwaka 2020 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa ambapo wanafunzi 65 walipata Divisheni 1 wanafunzi 49 divisheni 2 na divisheni 3 walikuwa 11.
Alisema,hata katika matokeo ya mwaka 2021 shule hiyo iliendelea kufanya vizuri kitaaluma kwa wanafunzi 61 kupata Divisheni 1,wanafunzi 51 walipata divisheni 2 na,wanafunzi 8 walipata divisheni 3.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.