Mkoa wa Ruvuma una ziada ya mahindi tani 326,497
MKOA wa Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2020/2021 umezalisha ziada ya mahindi tani 326,497 kati ya tani za mahindi 816,242 zilizozalishwa.
Akizungumza wakati anazindua soko la ununuzi wa zao la mahindi Kanda ya Songea mkoani Ruvuma katika kijiji cha Mgazini Halmashauri ya Songea,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema katika kipindi cha mwaka 2020/2021,wakulima wa mahindi wameweza kulima jumla ya hekta 276,488.
TAZAMA VIDEO YA UZINDUZI WA SOKO LA MAHINDI HAPA https://www.youtube.com/watch?v=j0jzllfFG0E&t=186s
"Uzalishaji huu ni zaidi ya kiwango kilichozalishwa kwa ongezeko la asilimia nne,ukilinganisha na kiwango cha uzalishaji katika msimu wa mwaka 2019/2020 ambapo tani 787,321 pekee zilizalishwa’’,alisisitiza Ibuge.
Brigedia Jenerali Ibuge amesema Mkoa una uwezo wa kuuza ziada hiyo ya mahindi ndani na nje ya nchi ambapo amewapongeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kwa uamuzi wa kununua mahindi ambayo ni sehemu ya ziada.
Amesema katika awamu ya kwanza ya ununuzi kutakuwa na vituo tisa katika Mkoa wa mzima ambavyo vimepangwa kwa lengo la kumrahisishia mkulima kuweza kununua mahindi yake bila kutumia gharama kubwa.
Hata hivyo amesema kiwango cha kununua tani 32,000 tu za mahindi kwa Mkoa wa Ruvuma ambacho kimewekwa na NFRA ni kidogo ukilinganisha na uzalishaji mkubwa wa mahindi uliofanywa na wakulima msimu huu.
Amesema mgawo huo ni kidogo hivyo ametoa rai kwa Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kuendelea kushirikiana kupanua wigo wa masoko ili wakulima wa Ruvuma waendelee kuzalisha ziada.
Ametoa rai kwa wanunuzi wengine nchini kote kufika mkoani Ruvuma kuendelea kununua mahindi ili kuipunguza ziada iende kwa wengine nje ya nchi na maeneo mengine yenye uhaba wa chakula ambapo amewaomba kununua kwa bei nzuri ili kuleta tija kwa wakulima na kuwawezesha kulima kwa tija zaidi.
Awali Meneja wa NFRA Kanda ya Songea Ramadhani Nondo alisema kwa ujumla NFRA katika msimu wa mwaka 2020/2021,wanatarajia kununua tani za mahindi 165,000 ambapo Kanda ya Songea imetengewa kununua mahindi tani 32,000 na kwamba kwa awamu ya kwanza zinanunuliwa tani 6,000 za mahindi.
Amesema mahindi yatanunuliwa kwa shilingi 500 kwa kilo katika kituo cha NFRA Ruhuwiko na vituo vingine mahindi yatanunuliwa kwa kilo shilingi 470 na kwamba ununuzi utafanyika kwenye vituo tisa vilivyopangwa ambavyo amevitaja kuwa ni Namtumbo mjini, Namabengo,Mgazini,Magagura,Mpitimbi,Mbinga mjini,Kigonsera na Ofisi za Kanda za NFRA Ruhuwiko.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho ameiomba serikali iongeze kiwango cha tani za ununuzi kwa sababu wananchi watauza kiasi kidogo cha mahindi ukilinganisha na uzalishaji,hivyo ameshauri serikali inunue mahindi kupitia mfuko mkuu wa serikali ili yakauzwe kwenye mahitaji ya chakula ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa wananchi wasipotafutiwe masoko ya uhakika ya mazao yao,wataendelea kupata hasara kwa kuuza kwa bei ndogo hali ambayo itawakatisha tamaa kuendelea kulima zao la mahindi.
Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka wa tatu mfululizo umeendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 16,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.