MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewasimamisha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuendelea na ujenzi jengo la Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
Mndeme amechukua uamuzi huo baada ya TBA kushindwa kukamilisha mradi huo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa,licha ya serikali kutoa zaidi ya shilingi bilioni 2.2 za utekelezaji wa mradi huo.
“Mimi silei wabadhirifu na wahujumu,Kuanzia leo hatuwaongezei tena muda,kuanzia sasa TBA,msimame ujenzi wa jengo hili na ujenzi wake utaendelea kwa kutumia force account,pia naagiza kuanzia leo TAKUKURU waanze kuchunguza mradi huu’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme amewaagiza TAKUKURU kuchunguza sababu za mradi huo kusuasua na kuchukua muda mrefu na kwamba iwapo kuna mtu yeyote amefanya hujuma dhidi ya mradi huo achukuliwe hatua haraka.
Amesisitiza haiwezekani jengo moja linachukua miaka zaidi ya mitatu hali ambayo inachelewesha maendeleo ya eneo husika,amelitaja lengo la Rais kutoa fedha hizo ni kutaka kuona watumishi wanafanyakazi katika mazingira rafiki na wananchi wanapata huduma katika mazingira bora.
Amewataka TBA wanapoomba kazi,kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati ambapo amesema licha ya kuongezewa muda wa mkataba mara mbili,bado wameshindwa kukamilisha mradi huo.
Amewatahadharisha TBA wasihangaike kuomba kazi za ujenzi ndani ya Mkoa wa Ruvuma kwa sababu miradi yote waliokuwa wanatekeleza ndani ya Mkoa wa Ruvuma wameshindwa kukamilisha.
Mndeme amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea kuhakikisha anasimamia mradi huo wakati,ambao sasa unakamlishwa kwa force account kwa wakati na viwango na kwamba serikali hivi sasa inatekeleza kwa wakati na viwango miradi mingi kwa force account.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya BICO Ahmed Nyange amesema mradi huo ambao umefikia asilimia 84 ulitarajiwa kukamilika Januari 20 mwaka huu,ambapo Mkandarasi aliongezewa miezi minne hadi Mei 31 mwaka,pia ameshinda kukamilisha mradi.
Nyange amesema hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi bilioni moja sawa na asilimia 61 ya gharama yote ya mradi na kwamba mkandarasi ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati ambapo amesema BICO inaunga mkono kukamilisha mradi kwa force account.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Shafii Kassim Mpenda amesema TBA imekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zinajitokeza mara kwa mara na kusababisha mradi kushindwa kukamilika kwa wakati.
“Nasikitika kusema kwamba imebidi tufikie hapa tulipofika ili kunusuru mradi na fedha za umma tusitishe mkataba na TBA na tuombe ridhaa kutoka kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI ili aridhie kukamilisha kazi zilizobaki kwa kutumia force account.
Awali Mwakilishi wa TBA Mhandisi Elias Tillya alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuwa walianza vizuri utekelezaji wa mradi huo na walitarajia Juni mwaka huu kukabidhi jengo hilo.
Hata hivyo amesema mwishoni mwa Mei mwaka huu TBA ilipata changamoto kwenye akaunti zake katika mikoa yote nchini hali ambayo ilisababisha kushindwa kutoa fedha baada ya akaunti zake zote kuzuiwa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 6,2020
Madaba
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.