Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezindua Kamati ya Maadili ya Mahakimu ngazi ya Mkoa katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mipango wa Mkoa mjini Songea.
Akizungumza kabla ya kuzindua kamati hiyo,Mndeme amesema mahakimu kama walivyo watumishi wengine wa umma,wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya sheria,kanuni na taratibu za nchi.
“Kwa muda mrefu watumishi wa kada ya mahakimu wamekuwa wakilalamikiwa kwamba wanakiuka maadili ya kazi yao kwa kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa,matumizi mabaya ya vyeo vyao na kutoa lugha isiyokuwa na staha mbele ya jamii na kutawaliwa na maslahi binafsi’’,alisisitiza Mndeme.
Hata hivyo Mndeme amesema vitendo visivyofaa vinavyofanywa na mahakimu wachache wasio waadilifu,vinachafua taswira ya mahakama na kwamba hali hiyo haifai kuacha kuendelea kushamiri.
Amelitaja jukumu kubwa la Kamati ya Maadili ni kuchunguza malalamiko yanayofikishwa mbele ya kamati na wananchi dhidi ya mahakimu ambapo ametoa rai kwa wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa umoja na mshikamano.
Mndeme amewaomba wananchi kuwasilisha malalamiko yenye ukweli mbele ya kamati ,pia amewaelekeza wakuu wa wilaya zote mkoani Ruvuma,kuunda Kamati za Maadili ya mahakimu ngazi ya wilaya ili kushughulikia malalamiko dhidi ya mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Kanda ya Songea Jaji Sekela Moshi,akizungumza kwenye uzinduzi huo,amesema mahakimu wana wajibu wa kutoa haki kwa sababu,mahakama imepewa mamlaka ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Hata hivyo Jaji Moshi amesema,inapotokea kuna ukosefu wa maadili ikiwemo utovu wa nidhamu,rushwa na mambo mengine,ndipo Kamati ya Maadili ya Mahakimu inachukua nafasi ya kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Amesema kupitia Kamati hiyo,wananchi wataelimishwa utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao ili kupunguza changamoto ya kuwasilisha malalamiko kwenye kamati husika.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki amesema,Kamati ya maadili ni jicho la Tume ya Utumishi wa mahakama katika kusimamia na kuimarisha nidhamu na maadili ya mahakimu.
Kamati ya maadili ya Mahakimu ngazi ya Mkoa inaundwa chini ya kifungu cha 50 cha sheria ya uendeshaji wa mahakama, ikijumuisha Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala wa Mkoa,Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa,wakili wa serikali Mfawidhi wa Mkoa na wajumbe wawili walioteuliwa na Jaji.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 8,2020
Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.