Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameongoza kikao kizito cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kutoa pongezi kwa halmashauri na watumishi waliosimamia vyema fedha za umma.
Akizungumza katika kikao hicho, Kanali Ahmed alisema ripoti ya CAG inaonesha Manispaa hiyo ina hoja 36, lakini ni hoja moja tu ndiyo iliyofungwa, huku 35 zikiwa bado wazi. Alitaka halmashauri zichukue hatua za haraka kuzifunga hoja hizo, ikizingatiwa 14 ni za miaka ya nyuma na 2 ni maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo hayajatekelezwa.
“Mchanganuo wa Katibu wa Baraza unaonesha kuna hatua zinazoridhisha, lakini hatupaswi kuridhika. Nataka halmashauri ziongeze kasi, zifanyie kazi hoja zilizosalia, na zifunge kabisa madhaifu yaliyobainika. Huu ni wajibu wetu kwa umma, kuonyesha uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma,” alisema Kanali Ahmed.
Mkuu wa Mkoa aliishukuru Ofisi ya CAG, madiwani, watumishi wa umma na wataalamu wa halmashauri kwa ushirikiano wa dhati. Alitambua juhudi zao za kuongeza mapato ya halmashauri, jambo linalochangia uboreshaji wa huduma kwa wananchi wa Ruvuma.
RC Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesisitiza uwajibikaji, uadilifu na umoja katika kusimamia rasilimali za umma. Hatua hizi si tu zinaboresha huduma kwa wananchi, bali pia zinajenga imani ya umma kwa taasisi za serikali. Mkoa wa Ruvuma unaendelea kusonga mbele, ukiweka misingi imara ya maendeleo, uwazi, na utawala bora.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, alisema mkoa umeendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa fedha za umma, hususan katika mwaka wa fedha 2023/2024. Amewapongeza watumishi mahiri, akisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya umoja, bidii na uadilifu wa watumishi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.