Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameungana na watoto yatima katika hafla ya chakula iliyofanyika katika makazi yake yaliyopo Manispaa ya Songea katika kuadhimisha sikukuu ya Idd.
Katika hafla hiyo, Kanali Ahmed amesisitiza umuhimu wa kuwatia moyo watoto wanaoishi katika mazingira magumu, akieleza kuwa idadi ya watoto hao katika mkoa ni zaidi ya 78,000.
Ameeleza kuwa idadi ya watoto hao ni kubwa na wanahitaji upendo na kushikwa mkono, hivyo wananchi wanapopata fursa ni vema kutembelea vituo vya watoto hao kuwasalimia na kuwapatia zawadi kwa kuwa watafarijika na wataweza kusoma kwa hamasa kubwa na kuweza kufikia malengo yao.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma, Victory Nyenza, amesema mkoa wa Ruvuma unawatambua watoto 78,337, kati ya hao watoto wa kiume ni 37,601 na wa kike ni 40,736.
Ameeleza kuwa watoto wote ambao wametambuliwa wameunganishwa kwenye huduma mbalimbali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kama vile huduma za msaada wa kisaikolojia, afya, elimu na malezi katika makao ya kuelekea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika hatua nyingine mlezi wa watoto yatima kutoka kituo cha Mt. Caterina kilichopo Mbinga, Sister Julietha, amesema watoto wameonyesha kufurahi kutokana na halfa hiyo ambayo imewakutanisha kutoka mazingira tofauti na kuwasaidia kusalimiana, kula chakula pamoja na kufarijiana.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.