Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wamiliki wa mashine za kuongeza virutubishi katika chakula wanapata elimu za urutubishaji wa chakula na kufungiwa mashine za kuongeza virutubishi.
Ametoa maagizo hayo wakati wa kikao kilicholenga kutoa Elimu kwa viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhusu uongezaji wa virutubishi kwenye chakula kilichofanyika katika ukumbi wa Hunt Club uliopo Ruhuwiko Manispaa ya Songea.
"Ili watoto wetu wafikie ukuaji timilifu na kuweza kutokomeza udumavu katika mkoa wetu, nitoe maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa wamiliki wa mashine waliopo kwenye halmashauri zenu wanapatiwa elimu ya urutubishaji wa chakula na kufungiwa mashine za kuongeza virutubishi ili waweze kuifikia jamii yetu kwa idadi kubwa," alisema Kanali Ahmed.
Maagizo mengine ni kufuatilia ili kuhakikisha urutubishaji vyakula unafanyika wakati wote ili kuleta matokeo mazuri katika kukabiliana na hali duni ya lishe.
Kanali Ahmed ameeleza kuwa hali ya lishe katika mkoa wa Ruvuma bado si nzuri hivyo amesisitiza umuhimu wa kuboresha hali ya lishe katika jamii hususan kwa watoto na wanawake ili mkoa na Taifa kwa ujumla liwe na jamii yenye siha nzuri.
Amebainisha kuwa hali ya udumavu katika mkoa ni asilimia 35.2, uzito pungufu asilimia 12.2, upungufu wa damu kwa watoto asilimia 45 na upungufu wa damu kwa wakina mama wajawazito ni asilimia 30, hivyo kutokana na hali hiyo mkoa umeendelea kuandaa mipango harakishi na shirikishi ya kupunguza udumavu kwa kushirikiana na wadau wanaoongeza virutubishi kwenye mazao lishe na unga wa mahindi ili kupunguza tatizo la madini na vitamin katika jamii.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Louis Chomboko, amesema kanuni zinawataka wasindikaji wote wa unga wa mahindi wanaofungasha kuongeza virutubishi ikiwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha viwanda vyote vinavyosindika unga wa mahindi vinarutubisha unga huo.
Amesisitiza umuhimu wa jamii kutumia chakula kilichoongezwa virutubishi kwa kuwa ndio kinga ya kuepuka athari zinazojitokeza kwa kukosa madini na vitamin zikiwepo watoto kuzaliwa na tatizo la kichwa kujaa maji, mgongo wazi, ukuaji duni kwa watoto kimwili na kiakili, ufupi, goita na upungufu wa damu mwilini.
Mkurugenzi wa kampuni inayojihusisha na teknolojia ya urutubishaji wa chakula (Sanku) upande wa Mashirikiano na Serikali, Gwao Omari Gwao, amesema asilimia kubwa ya jamii ya Ruvuma na watanzania wanatumia unga wa mahindi kutoka viwanda vidogo na vya kati ambavyo havijasajiliwa na haviongezi virutubishi kwenye unga wanaozalisha hivyo kuiweka jamii hatarini kiafya na lishe.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya mashine 937, kati ya hizo wanaofungasha ni 130, zinazoongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi ni 40 ambayo ni sawa na asilimia 31.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.