Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewaongoza wananchi kuaga miili ya watu sita waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Chunya Wilayani Mbinga.
Tukio hilo limefanyika katika uwanja wa michezo wa CCM uliopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga na kukabidhi miili hiyo kwa ndugu wa marehemu kwaajili ya kufanya maziko.
Akitoa salamu za pole wakati wa kuaga miili hiyo, Kanali Ahmed, amesema hiki ni kipindi kigumu na kinachoumiza hasa unapoangalia aina ya kifo kilichotokea, amewapa pole waliowapoteza wapendwa wao na kuwasihi watu wote kutumia msiba huo kutafakari maneno ya viongozi wa dini, kujiandaa kwa kusali, kufanya toba, na kushiriki kwenye matukio kama hayo kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa.
"Kuagana kwa aina hii hakuleti faraja hata siku moja, unaagana na mtu ambaye huwezi tena kukutana naye, ni kipindi kigumu, ni kipindi kinaumiza, kinaumiza zaidi unapoangalia aina ya kifo kilivyotokea, ndugu zetu hawa hawakuwa hata na dakika moja ya kujitetea, baadhi yao ni vijana wadogo walikuwa wana ndoto zao binafsi lakini Taifa lilikuwa lina ndoto kubwa dhidi yao, nimeyapokea haya kwa maumivu makubwa sana, na kwa idadi hii Mkoa na Taifa limepoteza nguvu kazi," alisema Kanali Ahmed.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amesema kutokana na ajali hiyo Shule ya Msingi Lumalu iliyokuwa na walimu watano imepoteza walimu wanne, hivyo watalifanyia kazi swala hilo ili wapate walimu wengine kwaajili ya kuendelea kutoa huduma shuleni hapo.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Komred Oddo Mwisho, amesema wananchi sita kuondoka kwa wakati mmoja ni idadi kubwa sana wakati bado walikuwa wanahitajika kulitumikia Taifa, hivyo Chama cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa kwa kuondokewa na nguvu kazi kubwa na aina ya kifo kilichowapata.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori amesema anaweza kuhisi maumivu wanayopata wafiwa Kwa kuwa wapo waliopoteza wazazi, watoto na wengine wake, amesema neno la Mungu likawape faraja wafiwa hao katika kipindi kigumu wanachopitia.
Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu sita ilitokea Disemba 28, 2024 katika kijiji cha Chunya wilayani Mbinga ilihusisha gari ndogo aina ya Prado ( T 647 CVR ) baada ya kupinduka na kuwaka moto, waliopoteza maisha ni walimu wanne wa shule ya msingi Lumalu ambao ni Damas Damasi Nambombe, Dominika Abehart Ndau, Judith Joseph Nyoni na John Silvester Mtuhi, dereva wa gari hiyo Vincent Alex Milinga pamoja na Raia mmoja Bonface Bosco Mapunda.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.