Katika juhudi za kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza kipato kwa wakulima, Mkoa umejipanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya parachichi na kahawa kwa kiwango kikubwa ifikapo mwaka 2025.
Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao anaitaja Mikakati hii inalenga kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo huku ikihamasisha wakulima kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa mazao haya yenye thamani kubwa sokoni.
Mapinduzi Katika Kilimo cha Parachichi
Kwa sasa, Mkoa unazalisha tani 1,768 za parachichi, lakini lengo ni kufikia tani 37,500 ifikapo mwaka 2025. Ili kufanikisha azma hii, Mkoa umeanzisha mkakati wa kuhamasisha wakulima kupitia vikundi mbalimbali vya kilimo.
Hadi sasa, juhudi hizo zimezaa matunda kwani tayari ekari 600 za parachichi zimekwishapandwa.
Mikakati hii inatekelezwa kwa kushirikiana na Taasisi ya SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania), ambayo inaunga mkono jitihada za wakulima kwa kuwapatia elimu ya kilimo bora, mbegu zenye ubora wa hali ya juu, na kuwaunganisha na masoko ya parachichi ndani na nje ya nchi.
Wakulima wanaendelea kufaidika na mwelekeo huu mpya wa kilimo cha kibiashara, ambao unawapa fursa ya kupata kipato endelevu.
Kahawa Yapewa Kipaumbele
Sanjari na juhudi za kuinua kilimo cha parachichi,Ngao anabainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma pia umeweka malengo makubwa katika kilimo cha kahawa.
Kwa sasa, Mkoa unazalisha tani 23,355 za kahawa safi, lakini matarajio ni kufanikisha uzalishaji wa tani 55,000 ifikapo mwaka 2025.
Kwa msimu huu, masoko ya kahawa yanaendelea kushamiri, huku vyama vya msingi vikiendelea kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo imekuwa ikihamasisha matumizi ya mbinu bora za kilimo cha kahawa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hili muhimu.
Mikakati hii ya Mkoa inaashiria mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, ambayo yatawanufaisha wakulima kwa kuongeza kipato chao na kuinua uchumi wa eneo husika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.