Mji wa mashujaa wa Songea , mkoani Ruvuma, shamrashamra za kumbukizi maalum za Mashujaa wa Vita ya Majimaji zimeanza kushika kasi, huku maandalizi yakiendelea kwa ajili ya tukio hili muhimu la kihistoria.
Kumbukizi hizi zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 23 mwezi huu, zikilenga kuwaenzi wapigania uhuru waliopambana dhidi ya ukoloni wa Kijerumani mnamo mwaka 1906 ambapo kwa mara ya kwanza kilele cha kumbukizi ya mashujaa wa Majimaji kitafanyika wilayani Namtumbo
Kwa wenyeji wa Ruvuma, kumbukizi hizi si tukio la kawaida bali ni sehemu muhimu ya kurithisha historia kwa vizazi vya sasa.
James Danny Mgego, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea, amesisitiza umuhimu wa wakazi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo.
“Tunapaswa kutambua na kuheshimu historia yetu. Mashujaa wa Vita ya Majimaji walitoa maisha yao kupinga ukandamizaji wa wakoloni, na ni jukumu letu kuhakikisha historia yao haipotei,” alisema Mgego.
Kwa upande wake, Rose Kangu, Kaimu Mfawidhi wa Makumbusho ya Majimaji, amehamasisha wananchi kuhudhuria maadhimisho haya ili kupata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu mashujaa hao.
“Hii ni historia yetu kama Taifa, na tunapaswa kuitunza kwa kuhakikisha kizazi cha sasa na cha baadaye kinajua mchango wa mashujaa wa Majimaji katika harakati za uhuru wa Tanganyika,” alisema Kangu.
Ratiba ya kumbukizi hizo imejaa matukio mbalimbali yenye lengo la kudumisha utamaduni na historia ya wapigania uhuru hao.
Kuanzia tarehe 23, shughuli rasmi zitaanza huku tarehe 24 ikitengwa kwa mashindano ya ngoma za asili za utamaduni. Vikundi vya sanaa kutoka maeneo mbalimbali ya Ruvuma vitashiriki katika kuonyesha utajiri wa tamaduni za wenyeji wa mkoa huo.
Tarehe 25, mdahalo mkubwa utafanyika Namtumbo, ambapo wanahistoria na wataalamu wa masuala ya ukombozi watajadili athari za Vita ya Majimaji na umuhimu wake katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hili ni tukio linalotarajiwa kuvuta hisia za wengi, hususan vijana wanaotaka kuelewa kwa kina historia ya ukombozi wa nchi yao.
Katika muendelezo wa maadhimisho hayo, tarehe 26 jamii ya Wangoni itakuwa na siku maalum ya kujifunza kuhusu tamaduni zao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurithisha mila na desturi kwa vizazi vya sasa.
Hatimaye, kilele cha kumbukizi hizi kitafanyika tarehe 27, ambapo shughuli mbalimbali za heshima kwa mashujaa wa Vita ya Majimaji zitafanyika. Katika siku hiyo, historia ya mashujaa hao waliopambana na hatimaye kunyongwa na wakoloni wa Kijerumani itasimuliwa kwa kina, ikikumbusha Watanzania umuhimu wa kujivunia urithi wao wa kishujaa.
Kwa wakazi wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla, kumbukizi hizi si tu tukio la kihistoria, bali ni fursa ya kutafakari juu ya thamani ya uhuru walioufurahia leo. Ni wakati wa kuenzi na kuheshimu waliotangulia kwa kujitoa mhanga, ili vizazi vijavyo viweze kuendelea kujifunza na kuthamini misingi ya Taifa lao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.