Mkoa wa Ruvuma umeandika historia mpya baada ya kuadhimisha Siku ya Uchangiaji Damu Duniani kwa mafanikio makubwa, huku viongozi wa serikali, taasisi na wananchi wakijitokeza kwa wingi kuunga mkono zoezi hilo la kuokoa maisha.
Akihutubia umati wa wananchi katika viwanja vya Manispaa ya Songea, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Michael Mbano, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, alisema kaulimbiu ya mwaka huu “Changia damu, leta matumaini — pamoja tunaokoa maisha” inabeba wito wa umoja na mshikamano wa jamii.
Mbano alisema kuwa, kuanzia Januari hadi Juni 12, 2025, mkoa umekusanya chupa 4,040 za damu, ikiwa ni asilimia 27 ya lengo la mwaka mzima. Alibainisha kuwa mafanikio haya yamekuja kutokana na hamasa ya wananchi, taasisi, na dini, waliojitokeza kuchangia bila kusita.
Akielezea mikakati ya serikali, Mbano alisema huduma za afya zinaimarika siku hadi siku, kupitia uboreshaji wa majengo, upatikanaji wa vifaa tiba, dawa, na mashine za uchunguzi, lengo likiwa ni kuhakikisha damu salama inapatikana kwa wote wanaohitaji.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vituo 37 vinavyotoa huduma ya damu, kati ya hivyo 26 vinamilikiwa na serikali, 11 vinamilikiwa na taasisi za dini, hali inayochochea upatikanaji wa damu salama na ya kutosha. Mbano alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanafunzi wa shule, vyuo, taasisi za dini, mashirika ya kiraia, na jamii kwa ujumla kuendelea kuchangia damu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Chioma Mhako, alibainisha kwamba, kati ya Juni 1 hadi 13, 2025, mkoa umekusanya chupa 1,213 za damu, idadi inayovuka lengo la chupa 1,035 kwa kipindi hicho. Dkt. Mhako aliwashukuru wananchi kwa moyo wa huruma na mshikamano wa kuokoa maisha ya wenzao.
Mafanikio haya ya Mkoa wa Ruvuma ni kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa jamii, pale inapoungana kwa lengo la kuokoa uhai wa binadamu. Huu ni wito kwa mikoa mingine kuiga mfano wa Ruvuma, na kwa Watanzania wote kuendelea kuchangia damu, kwani tone moja la damu linaweza kuokoa maisha ya mtu aliye hatarini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.