Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, umeanza kutekeleza programu ya uchimbaji wa visima 900 nchini, ambapo kila jimbo linapata visima vitano.
Katika Wilaya ya Tunduru, yenye majimbo mawili ya Uchaguzi—Tunduru Kusini na Kaskazini—jumla ya visima 10 vinachimbwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 600.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa RUWASA Wilaya ya Tunduru, Leticia Mwageni, amesema mradi huo unalenga vijiji ambavyo havina miradi ya maji ya bomba ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Miongoni mwa vijiji vinavyonufaika ni kijiji cha Angalia, kata ya Mtina, ambacho kinapata kisima kinachojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 60 kwa kutumia mafundi wa ndani.
Mwageni ameeleza kuwa RUWASA imenunua vifaa vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Tayari ujenzi wa kituo cha kuchotea maji (kioski) umeanza, na matarajio ni kwamba ndani ya mwezi mmoja wananchi wataanza kupata maji safi na salama.
“Wilaya ya Tunduru ina majimbo mawili—Tunduru Kusini na Kaskazini—ambapo Jimbo la Tunduru Kusini limepata visima vitano kwa gharama ya shilingi milioni 300, huku Jimbo la Tunduru Kaskazini likipata visima vitano pia,”
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Angalia, Ramadhan Nyenje, ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo wa maji katika kijiji hicho ambacho hakijawahi kuwa na maji ya bomba tangu Uhuru mwaka 1961.
Amesema kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 6,332 kilikuwa kinategemea vyanzo vya asili kama mito na mabonde, ambavyo havitoshelezi mahitaji yao.
Ameongeza kuwa mradi huo utasaidia kupunguza muda wa kusubiri maji kwenye mabomba machache, na kwa kuwa ujenzi wake uko karibu na Shule ya Msingi ya kijiji hicho, wanafunzi watafaidika kwa kupata maji safi ya kunywa, kupikia na kusafisha mazingira yao.
Mkazi wa kijiji cha Angalia Zena Ismail, ameiomba RUWASA kuharakisha ujenzi wa mradi huo na kuweka mabomba kwenye makazi yao ili maji yaweze kufika majumbani, badala ya kutegemea vituo vya kuchotea maji.
Amesema kwa sasa wanategemea vyanzo vya maji vya asili ambavyo siyo salama, lakini hawana mbadala, hivyo mradi huo utawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.