WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji ametaka kuwepo na mabadiliko makubwa ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma kuhakikisha kwamba wakulima wadogo wanaunganishwa katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
Alisema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa maandalizi ya Kongamano la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRF), litakalofanyika nchini Rwanda mwezi ujao ambapo pia Rais Samia Suluhu Hassan anategemewa kuhudhuria.
Katika kongamano hilo la Rwanda, Tanzania inatarajiwa kueleza nafasi ya uwekezaji na kuwakutanisha wafanyabiashara wake na wengine wa kimataifa. Kwa kawaida mkutano huo huwa na fursa nyingi za biashara na uwekezaji.
Akizungumzia maandalizi hayo ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRF) 2022 litakaloanza Septemba 5-9, 2022 nchini Rwanda, alisema serikali inaendelea kuimarisha ushiriki wake katika kilimo kwa kukifanya kuwa injini ya kunyanyua uchumi na sekta binafsi lazima ifanye kazi yake ikiwamo kuwekeza katika maeneo ambayo yanaleta athari chanya katika kuimarisha kilimo.
Dk Ashatu alitoa wito kwa wadau wa kilimo ikiwamo sekta binafsi na sekta za umma kutumia mkutano huo kwa ajili ya kupanga kitu ambacho wanataka kukifanya kwenye mkutano huo wa Kigali.
Alisema katika mkutano huo kwamba Tanzania imepata nafasi ya kujiuza kwa jumuiya ya kimataifa hivyo wajasiriamali katika sekta ya kilimo na biashara ya kilimo wanatakiwa kuunganisha nguvu na kuja na msimamo wa pamoja wenye kusaidiana kukibadili kilimo.
Alisema serikali katika kuimarisha kilimo imeweka mazingira safi ya uwekezaji, imeondoa tozo mbalimbali na kuleta nafuu katika pembejeo na kutaka washiriki wa mkutano huo kuona maeneo ambayo yanastahili kurekebishwa ili kubadili kilimo cha Tanzania na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na kuzalisha kwa ziada kwa ajili ya dunia.
Alisema katika mkutano huo anaamini kwamba washiriki pia wataangalia na kutambua sera zinazokwamisha kasi ya mabadiliko katika kilimo na kuishauri serikali namna ya kufanya.
Aidha, amewataka kuangalia maeneo ambayo yanaweza kushirikisha moja kwa moja sekta binafsi yenyewe kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa kutumia changamoto zilizopo duniani kuleta ustawi.
Katika kuinua kilimo kinachotegemewa na asilimia 65 ya wananchi ametaka sekta binafsi na umma kuangalia kilimo kwa nia ya kushawishi vijana washiriki kwa kuona wapi wakulima wadogo wanaweza kupata fedha rafiki kwa ajili ya kubadili kilimo chao.
Waziri alihoji wapi sekta binafsi inakwama katika kusaidia serikali ama yenyewe katika kutumia fursa zilizopo kuhudumia duniani hasa kwa kuzingatia jiografia ya Tanzania duniani kama lango la chakula kwa jamii nyingine.
"Nini tunachotakiwa kukinyanyua kama serikali ili tuihudumie dunia kutoka Tanzania," alihoji Dk Ashatu huku akiongeza kwamba lengo la Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia ni kuhudumia dunia kutoka Tanzania na kwamba lazima kujifunza nini wanaweza kusema Kigali ili kuboresha kilimo.
Alisema kilimo ni ajira na hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba kinafunguliwa na kutumika kuleta maendeleo kwani kwa sasa kina tija kidogo, hali inayoweza kusababishwa na ufahamu mdogo wa washiriki wa sekta hiyo kuhusu namna ya kuendesha kilimo cha kisasa.
Kwa kuzingatia mkutano wa Kigali, aliwataka wawakilishi wote kujadili na kwenda na maazimio yatakayokuwa kama msimamo wa nchi huku mambo wanayokwenda kuyatafutia uwekezaji na soko kuwa ni sekta ya maziwa, ufugaji samaki, kilimo cha mboga na matunda na mafuta ya kula.
Naye Makamu wa Rais wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), Dk Apollos Nwafor alipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwa makini katika mipango ambayo imelenga kubadili kilimo.
Alisema Rais Samia ameonesha nia katika kubadili kilimo cha Tanzania kwa kulenga zaidi mfumo imara na endelevu wa uzalishaji wa chakula.
Alisema taasisi ya Agra inaangalia juhudi za Rais Samia katika mawanda mapana zaidi kwa kuwa mfumo wa chakula duniani hutegemea zaidi nchi mbalimbali zinavyotekeleza malengo ya Umoja wa Mataifa ya usalama wa chakula.
Alisema kilimo kikiwa injini ya kukuza uchumi juhudi lazima zifanyike kubadili kilimo na kukifanya kuwa cha kibiashara.
Alisema kwa sasa dola za Marekani bilioni 50-60 hutumika kila mwaka kwa ajili ya kuingiza chakula barani Afrika hivyo kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika kilimo.
Alisema mkutano wa Kigali, Rwanda umelenga kuhakikisha nchi washiriki wanakuwa na nafasi ya kushawishi uwekezaji katika kilimo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.