Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema serikali imefanyya juhudi kubwa za kuleta magari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) ili kuimarisha huduma za rufaa za wagonjwa hasa mama na mtoto.
Kanali Abbas amesema hayo wakati anazungumza katika makabidhiano ya mwendelezo wa mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa akina mama wajawazito (M-mama) kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amesema hivi sasa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya magari ya kubeba wagonjwa 21 kati ya hayo magari 15 ni mapya kabisa.
“Natambua kuwa kiuhalisia magari ya kubebea wagonjwa yaliyopo hayawezi kutosheleza mahitaji ya kusafirishia rufaa kutoka pande zote za Mkoa wetu kutokana na sababu mbalimbali,hivyo pengo hili litaendelea kuzibwa kwa kuwatumia madereva ngazi ya jamii ambao wamesaini mikataba katika Halmashauri zetu’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto lengo likiwa ni kupunguza na kumaliza tatizo la vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya Watoto wachanga vinavyozuilika.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri zote mkoani Ruvuma kusimamia mfumo wa M-mama kwa kuhakikisha magari ya wagonjwa yanakuwa tayari wakati wote na kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa madereva ngazi ya jamii na kusimamia kuharakisha malipo yao kulingana na mikataba.
Kanali Abbas amewaelekeza wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Halmashauri zimetenga bajeti zitakazowezesha utekelezaji wa shughuli za rufaa kila mwaka na kuendelea kuweka fedha kwenye akaunti kuu ya Taifa ya m-mama iliyoanzishwa na serikali.
Naye Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Hilda Ndambalilo ameutaja mfumo wa M-mama kuwa ni mfumo wa usafirishaji wa dharura wa akinamama wajawazito waliojifungua ndani ya siku 42 na Watoto wachanga wa siku 0 hadi 24.
Amesema katika mfumo huo ambao ulizinduliwa mkoani Ruvuma Mei 2023,hadi sasa umewezesha kusafirisha jumla ya wagonjwa 1,938 kati yao akinamama wajawazito 1,664 na Watoto wachanga 274.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.