WANANCHI wa vijiji vilivyopo katika Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wamesisitizwa kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali zinazojengwa na Serikali kwenda kufanya uchunguzi wa afya zao na kupata huduma za matibabu.
Rai hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mbinga Dkt Seleman Jumbe,wakati wa ziara yake ya kutembelea vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo ujenzi wa mradi wa wodi ya wanawake,watoto na wanaume yanayojengwa katika Hospitali ya Halmashauri iliyopo kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga.
Alieleza kuwa,wananchi wanatakiwa kuhakikisha wanatumia vituo na Hospitali hizo kupata huduma kwa kuwa fedha zinazotumika kutekeleza miradi hiyo zinatolewa na Serikali yao na wanapaswa kujivunia na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
Dkt Jumbe alisema kuwa,Serikali imetoa Sh.milioni 850 kati ya hizo Sh.milioni 500 zimepangwa kutumika kujenga wodi tatu ambazo ujenzi wake upo hatua ya kufunga milango,madirisha na kuweka malumalu na Sh.milioni 35 kwa ajili ya kununua vifaa tiba.
“Mbali na fedha hizo Mheshimiwa Rais Samia ametupatia fedha nyingine Sh.milioni 300 ili kujenga jengo la upasuaji,kwa sasa tupo katika hatua za manunuzi ili kumpata mzabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi”alisema Dkt Jumbe.
Alisema,mpango wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Halmashauri ya wilaya Mbinga ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu kwenye maeneo yao ili kuwaondolea adha ya kwenda mbali kufuata huduma za afya.
Alisema,Hospitali ya Halmashauri kwa sasa inahudumia zaidi ya wakazi 60,000, hata hivyo matarajio yao majengo mapya yatakapokamilika idadi ya wananchi itaongezeka kutokana na uwepo wa huduma muhimu ikiwemo za upasuaji.
Kwa mujibu wa Dkt Jumbe,Halmashauri ya wilaya Mbinga kuna vituo 8 vya afya,lakini mkakati uliopo kujenga vituo vingine kwa kila kata na wameanza kujenga vituo viwili katika kata ya Linda na Mkumbi ambapo ujenzi wake unaendelea vizuri.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga Dkt Salum Bundala,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha zilizowezesha kujenga majengo matatu ya wodi ya akina mama,wanaume,watoto na jengo la utawala ambayo yakikamilika yataondoa adha iliyopo ikiwemo ukosefu wa wodi ya kulaza wagonjwa.
Alisema, wanalazimika kutumia moja ya majengo yaliyopo kwa ajili ya kulaza wagonjwa na mama wajawazito wanatumia moja ya jengo la wagonjwa wa nje kwa ajili ya kupata huduma za uzazi na kujifungua na wagonjwa wengine watapata wodi ambayo itasaidia kupunguza msongamano wanapofika kupata matibabu.
Kaimu katibu wa afya Dickson Simangwe alitaja majengo yaliyokamilika katika Hospitali hiyo ni jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara,jengo la kufulia,jengo la kutunzia dawa na vifaa tiba,kichomea taka,jengo la wagonjwa mahututi,utawala na jengo la mionzi.
Alitaja vituo vipya vinavyojengwa na gharama zake ni kituo cha afya Mkumbi(500 ml)kupitia fedha za tozo,kituo cha afya Nyoni(500ml)kutoka mapato ya ndani,kituo cha afya Linda(179ml mapato ya ndani.
Alisema,kituo cha afya Kindimbachini kinachojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 500 fedha kutoka Serikali kuu ambapo itahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje,maabara,jengo pacha la huduma za uzazi,upasuaji,jengo la kufulia na kichomea taka na wamepokea Sh.milioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya kuishi watumishi watatu(Three in one).
Alitaja vituo vilivyokamilika na kuanza kutoa huduma ni kituo cha afya Litumbandyosi kilichojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 598 kupitia mapato ya ndani na kituo cha afya Matiri kilichogharimu Sh.milioni 500.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera Rehema Mbele,ameiomba Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Mbinga kumaliza ujenzi wa majengo mapya ili waweze kupata baadhi ya huduma ikiwemo ya kulaza wagonjwa na upasuaji ambazo hazipatikani katika Hospitali ya wilaya.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Semen Ndunguru alisema,matarajio yao pindi majengo hayo yakikamilika watapata huduma za matibabu karibu badala ya kuendelea maeneo mengine.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.