Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema serikali imejidhatiti kuhakikisha wananchi wanapata umeme hususani katika vitongoji, na vitongoji 557 vya Mkoa wa Ruvuma vitanufaika.
Akizungumza katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, ameeleza kuwa Tanzania ina vitongoji takribani 64,000, na hadi sasa wamefanikiwa kupeleka umeme kwenye vitongoji 33,000.
Amesema wakati serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaingia madarakani, kulikuwa na vijiji 4,071 visivyokuwa na umeme, ameeleza kuwa ilani ya Chama cha Mapinduzi iliagiza kukamilisha zoezi la kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2025, na hadi sasa zoezi hilo limekamilika.
Mhe. Kapinga amebainisha kuwa serikali sasa inaelekeza nguvu katika kuhakikisha umeme unafika kwenye vitongoji ambapo vitongoji 557 katika mkoa wa Ruvuma vitanufaika na mradi huo wa kufikishiwa umeme katika awamu ya kwanza ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitanabaisha katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo ameeleza kuwa kila mmoja anahusika katika kuhakikisha maono ya Rais yanafikiwa, ifikapo mwaka 2030, asilimia 75 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, na asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Amesema tafiti zilizofanywa zimeonyesha kuwa matumizi ya nishati safi ni rahisi zaidi kuliko matumizi ya nishati isiyo safi kama mkaa na kuni, ambazo gharama zake ni kubwa ukilinganisha na nishati safi ambapo Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi kwa manufaa ya afya na mazingira.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.