Sasa wagonjwa kupata huduma bobezi za kibingwa ndani ya Mkoa wa Ruvuma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imekabidhi vifaa vya tiba mtandao katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma hali ambayo itawawezesha wananchi kupata huduma bobezi za kibingwa ndani ya Mkoa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma,Mwakilishi wa Wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa Tiba Mtandao,Dr. Ligile Vumilia amesema huduma hiyo ni muhimu hasa kwa wananchi wanaoishi pembezeni kama Mkoa wa Ruvuma.
Amesema wananchi wote ambao watakuwa wanahitaji huduma za afya za kibingwa na bobezi sasa watazipata katika hospitali ya Rufaa ya Ruvuma badala ya kusafiri umbali mrefu ambapo serikali imeichagua hospitali hiyo kuwa ni miongoni mwa hospitali tano za mwanzo kabisa nchini kupatiwa huduma hiyo.
Dr.Vumilia amesema kuletwa kwa vifaa hivyo katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma ni kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipofanya uzinduzi wa X-Ray katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mwaka 2019,aliagiza kuanzisha huduma ya tiba mtandao katika hospitali hiyo.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya imeichagua Hospitali za Rufaa za Ruvuma,Bombo Tanga, Mkoa wa Katavi na hospitali mbili za Wilaya za Nzega na Chato kuwa hospitali za mwanzo kufungiwa huduma ya tiba mtandao’’,alisisitiza Dr.Vumilia.
Amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa wote umetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununua vifaa tiba mtandao kwa ajili ya hospitali tano nchini na kwamba vifaa vya tiba mtandao vinapelekwa katika hospitali hizo na vitaunganishwa kwajili ya kuanza kazi ya kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa.
Hata hivyo amesema Taasisi ya Teknolojia nchini inatarajia kufunga vifaa vya tiba mtandao baada ya makabidhiano hayo ambapo katika hospitali ya Rufaa ya Ruvuma chumba maalum kimeshaandaliwa kwa ajili ya kufungwa vifaa hivyo.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo,huduma hiyo inatarajiwa kutolewa katika hospitali za Rufaa 21 nchini na kwamba huduma ya tiba mtandao katika hospitali hizo itaunganishwa na hospitali za Kanda za Bugando Mwanza,Kanda ya Benjamin Mkapa Dodoma na Kanda ya Mbeya.
“Tutakuwa na hospitali nne za kitaifa ambazo zitakuwa na huduma bobezi za kibingwa ambazo ni hospitali ya Taifa Muhimbili,hospitali ya mishipa na mifupa ya fahamu ya MOI,hospitali ya saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Jakaya Kikwete ambayo ni maalum kwa magonjwa ya moyo’’,alisisitiza Dr.Vumilia.
Amesema huduma ya tiba mtandao katika hospitali ya Rufaa ya Ruvuma itamwezesha mgonjwa yeyote kupata huduma bobezi za kibingwa bila kusafiri umbali mrefu kama hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma Dr.Magafu Majura amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa vifaa vya tiba mtandao ambao utawawezesha wananchi kufanyiwa vipimo mkoani Ruvuma na vipimo hivyo kutumwa kwa njia ya mtandao hivyo mgonjwa kufahamu ugonjwa wake akiwa Ruvuma hivyo kupunguza gharama za usafiri na malazi kwa mgonjwa.
“Kwa kutumia vifaa vya tiba mtandao tutakuwa sawa na waliopo Dar es salaam,wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na nchi jirani za Msumbiji na Malawi sasa watapata huduma za kibingwa wakiwa Songea’’,alisisitiza Dr.Majura.
Naye Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Afya Catherine Sungura amesema serikali pia imetoa shilingi milioni 630 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma na kwamba katika nchi nzima serikali inajenga majengo ya wagonjwa wa dharura katika hospitali nane za rufaa.
Sungura amesema pia serikali imetoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ambapo miradi yote hiyo imetekelezwa kwa asilimia 100.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Machi 23,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.