Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya barabara mkoani Ruvuma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa,kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ,Kanali Abbas amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa maendeleo ya miundombinu ya barabara.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, tangu mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya Tsh. Bilioni 179.282 kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara katika Mkoa wa Ruvuma.
“Kati ya fedha hizo, Tsh. Bilioni 76.098 zilitolewa kwa TANROADS Ruvuma na Tsh. Bilioni 103.184 kwa TARURA Ruvuma”,alisema
Amesema Kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, TANROADS Ruvuma imeidhinishiwa bajeti ya Tsh. Bilioni 17.964, huku TARURA Ruvuma ikipata Tsh. Bilioni 38.294.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa fedha hizo zinaonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha sekta ya barabara kwa maendeleo ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa TANROADS na TARURA kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi ili kutoa matokeo chanya kwa wananchi wa Ruvuma.
Alisisitiza umuhimu wa kuweka mpango kazi shirikishi wa kimkoa ili kuleta tija katika utekelezaji wa miradi ya barabara.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya barabara nchini, akisema kuwa hatua hizo zinaimarisha maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla .
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amesisitiza suala la utunzaji wa barabara ambapo ameziagiza mamlaka zinazohusika zikiwemo Halmashauri zihakikishe zinasimamia matumizi bora ya barabara, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha magari ya mizigo yakiwemo magari ya makaa ya mawe kutoshusha makaa ya mawe kwenye sehemu za hifadhi ya barabara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.