Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga shilingi bilioni 216 kwa ajili ya zoezi la utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo katika mikoa yote nchini kwa kipindi cha miaka mitano.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Meena, ametoa taarifa hiyo wakati wa kushuhudia utoaji wa chanjo kwa mifugo katika shamba la Jenista Mhagama lililopo Kijiji cha Mpandangindo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, ikiwa ni kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha utoaji wa chanjo kwa mifugo.
Amesema kuwa zoezi la utoaji wa chanjo ni endelevu na kwamba chanjo hizo zimetolewa na Serikali kwa ruzuku, hivyo ni salama kwa matumizi, akiwahimiza wafugaji kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao ili kuepuka magonjwa hatari kwa mifugo.
Bi. Meena ameongeza kuwa Serikali imelenga kuchanja ng’ombe milioni 19 au zaidi, mbuzi na kondoo milioni 17 au zaidi, pamoja na kuku wa kienyeji milioni 40 au zaidi ifikapo Septemba 2025, ikiwa lengo ni kuboresha afya ya mifugo, kuongeza kipato cha wafugaji na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yanayovuka Mipaka kutoka Wizara hiyo, Dkt. Daniel Mdetele, amesema kampeni hiyo inalenga kukabiliana na magonjwa yanayoathiri uzalishaji na biashara ya mifugo.
Amezitaja chanjo zinazotolewa kuwa ni dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo, pamoja na chanjo ya 3-in-1 kwa kuku wa kienyeji inayodhibiti mdondo, ndui na mafua ya ndege kwa wakati mmoja.
Naye Katibu wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Ruvuma, Prisca Kaponda, amesema wafugaji wa mkoa huo wako tayari kushiriki kikamilifu katika zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo yao.
Vilevile Ndugu Jumanne Mwankhoo, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, amesema wanaamini kuwa kila mfugaji atafikiwa katika kampeni hiyo ili kuhakikisha mifugo yote inapata chanjo stahiki.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.