SERIKALI imetoa kiasi cha Zaidi ya Shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali, vituo vya afya, zahanati pamoja na nyumba za watumishi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge wakati anataja mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea.
Amesema Serikali imetoa Zaidi ya Bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya eneo la Mwengemshindo Songea Manispaa lenye ukubwa wa hekta 265.
‘’Niseme pia ujenzi wa vituo 13 vya afya unaendelea na fedha zimekua zikitumwa hadi sasa tumepokea Zaidi ya Bilioni tatu kupitia fedha za tozo lakini pia za mapato ya ndani ya Halmashauri zetu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo’’, amesema RC Ibuge.
Amesema Mkoa umepokea jumla ya shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu ya huduma za dharura.
Hata hivyo RC Ibuge ameongeza kuwa Mkoa umetengewa jumla ya shilingi Milioni 840 kwa ajili ya kununua mashine mbili za mionzi.
Amesema katika mapambano dhidi ya UVIKO 19 Mkoa umefanikiwa kuchanja watu 277,645 sawa na asilimia 32 ya lengo la kuchanja watu 670,557, kati ya waliochanjwa watu 214,004 sawa na asilimia 77.1 wamekamilisha dozi zote na watu 63,641 sawa na asilimia 22.9 wamekamilisha dozi ya kwanza.
Mkoa wa Ruvuma umeongoza kitaifa katika zoezi la utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 tangu zoezi la utoaji lilipoanza hadi sasa.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Aprili 04 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.