SHAMBA la miti Mpepo linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wilayani Nyasa mkoani Ruvuma limefanikiwa kupanda miti hekta 2,240.
Akitoa taarifa ya shamba hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo John Kimolo amesema kati ya hekta zilizopandwa,hekta 1440 zimepandwa miti jamii ya misindano (pines) katika tarafa ya Mpepo wilayani Nyasa na Liwilikitesa wilayani Mbinga.
Kimolo amebainisha zaidi kuwa hekta 400 imepandwa miti jamii ya misaji (teak) katika eneo la Liuli mwambao mwa ziwa Nyasa na kwamba miundombinu ya bustani tayari imesimikwa kwa ajili ya uzalishaji wa miche ya misaji katika maeneo ya Liuli na Ndongosi.
“Shamba lina bustani nne Mpepo,Ndongosi,Tunduru na Liuli yenye jumla ya miche ya miti1,130,000 ikijumuisha miche aina ya misindano na misaji’’,alisisitiza Kimolo.
Kulingana na Mhifadhi Mkuu huyo,shamba la miti Mpepo ni miongoni mwa mashamba 24 yanayosimamiwa na kuhudumiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na kwamba shamba hilo lilianzishwa 2017/2018 likiwa na ukubwa wa hekta 2,017 ambapo hivi sasa shamba hilo lina ukubwa wa hekta 20,905.
Hata hivyo Kimolo amesema Shamba la miti Mpepo limefanikiwa kupata eneo lenye ukubwa wa hekta 50,000 wilayani Tunduru kwa ajili ya uanzishwaji wa shamba jipya la miti ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga bajeti ya kuanza upandaji miti hekta 100.
Amezitaja faida za shamba hilo kuwa ni chanzo cha mapato ya serikali kuu,kupatikana kwa ajira za muda 3000 kwa mwaka,Halmashauri kupata tozo mbalimbali na upatikanaji wa malighafi za viwandani.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya shamba hilo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewapongeza TFS kwa kufanya kazi kubwa ya kupanda miti ambayo amesema ni biashara kubwa kutokana na mahitaji makubwa ya mbao.
“Kilimo ambacho kinaondoa umasikini kwa haraka lakini kinahitaji Subira ni kilimo cha upandaji wa miti,ukiwa na hekari moja ya miti,baada ya miaka 15 utakapoanza kuvuna miti,ndipo utaona faida kubwa ya kilimo cha miti’’,alisisitiza RC Thomas.
Amesema maeneo mengi ambako wanapanda miti kibiashara wamepata maendeleo makubwa hivyo ametoa rai kwa wananchi mkoani Ruvuma kuwa sehemu ya wapandaji wa miti badala ya kuwaachia TFS pekee.
Hata hivyo katika kukabiliana na uchomaji moto hovyo,Mkuu wa Mkoa amewaasa wananchi kuacha tabia ya kuandaa mashamba yao kwa kutumia moto badala yake watumie njia nyingine ambazo hazina madhara kwenye misitu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 20,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.