Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amewaongoza wananchi wa Wilaya ya Songea kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, ambapo tarehe 26 Aprili 1964 nchi ya Tanganyika na Zanzibar ziliungana.
Maadhimisho hayo ambayo yalitanguliwa na shughuli mbalimbali kama upandaji wa miti na usafi wa mazingira katika Wilaya ya Songea, yalianza kwa maandamano ya amani na kuhitimishwa kwa hafla fupi katika viwanja ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Songea iliyopo manispaa ya Songea.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Ndile, amesema wananchi wanapaswa kujua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni jitihada za watu na viongozi wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika ili kulifanya Taifa liwe moja, lenye watu wanaoheshimiana, wanaoelewana na kuthaminiana utu.
Ameongeza kuwa kama Taifa linatakiwa kujivunia umoja na mshikamano uliopo baina ya watu wote nchini bila kujali desturi na maeneo wanayotokea kwa kuwa ndio msingi imara wa amani katika Taifa.
Ametoa wito kwa watumishi wa umma na wananchi wote kuwa watiifu na waaminifu kwa Taifa na kuepuka kutoa kauli ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani ili kuhakikisha Taifa linaepuka machafuko yayiso na msingi.
Akitoa historia ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa Wazee Wilaya ya Songea, Sofia Namananda, amesema waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume, walikuwa na maono ya mbali katika kuhakikisha nchi inakuwa na mshikamano na umoja wa kujenga Taifa Moja la Tanzania.
Ameeleza kuwa hivi sasa Taifa linajivunia matunda ya nguvu walizotumia waasisi hao, kwa kuwa walifanya kazi kubwa mpaka hivi sasa wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo wanaliombea Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.
Kwa upande wake Mkazi wa Wilaya ya Songea, Mohamed Kwizombe, amesema maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania kama mwananchi anajivunia amani na utulivu uliopo katika Taifa hivyo amani idumishwe hadi kufikia vizazi vijavyo.
Maadhimisho hayo ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, ambao ulifanyika Arili 26, 1964 na kuasisiwa na Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume, kwa mwaka huu wa 2025 yameongozwa na kauli mbiu inayosema " Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa , Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025".
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.