Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Ruvuma limewahakikishia wakazi wa mkoa huo kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme itatatuliwa kabisa. Hii ni kutokana na mpango wa kubadilisha nguzo za umeme za miti na kuweka nguzo za zege ili kuboresha huduma.
Afisa Msaidizi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Ruvuma, Emma Ulendo, amesema shirika hilo limejikita katika kuboresha miundombinu ya umeme kwa kuondoa nguzo chakavu na kuweka za zege, ambazo ni imara na bora zaidi. Alizungumza kupitia Jogoo FM Februari 11, 2025, akiwahakikishia wananchi kuwa huduma itaendelea kuimarika.
Kwa sasa, TANESCO imeboresha huduma kwa wateja kwa kuweka mafundi katika kila kata, mijini na vijijini, ili kuhakikisha matengenezo yanafanyika haraka.
Aidha, Emma amewataka wananchi kuwa waangalifu na matapeli wanaojitambulisha kama wafanyakazi wa TANESCO na kuwalaghai kwa kuomba fedha. Amehimiza wateja kutoa taarifa kupitia simu, WhatsApp, au ofisi za TANESCO kwa hatua za kisheria kuchukuliwa.
Kwa upande mwingine, TANESCO inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya umeme na nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa mijini na vijijini, ili kuondoa dhana kwamba umeme ni ghali na kuwahamasisha kutumia nishati safi kwa maendeleo endelevu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.