WAKAZI wa kijiji cha Ngapa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na wakazi wa kijiji cha Kilimalondo wilaya ya Nachingwea Mkoa wa Lindi,wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kujenga daraja katika Mto Lumesule ili kuwanusuru wasiendelee kupoteza maisha kwa kusombwa na maji na kurahisisha mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili.
Charles John Mkazi wa kijiji cha Kilimalondo wilayani Nachingwea amesema,daraja katika Mto huo lina umuhimu mkubwa kwani litawawezesha kuwa na mawasiliano ya uhakika majira yote ya mwaka na kufanya shughuli za usafi na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Amesema,pindi maji yanapojaa katika mto huo ambao ni mpaka wa mikoa ya Ruvuma na Lindi,wanalazimika kutumia gharama kubwa kati ya Sh.5,000 kwa mtu na Sh.15,000 kuvusha pikipiki pindi wanapotaka kuvuka kwenda upande mwingine.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ngapa Yasin Likenge ameishauri serikali, kuacha kusubiri hadi watu waendelee kupoteza maisha ndipo ijenge daraja katika eneo hilo, badala yake ione umuhimu wa kujenga daraja haraka ili kunusuru maisha ya wananchi wake.
Mhandisi kutoka Ofisi ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Irene Kapinga amesema,TANROADS imeanza maandalizi ya kujenga daraja katika mto Lumesule ili kuunganisha mawasiliano ya wananchi wa wilaya mbili za Nachingwea na Tunduru mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa Kapinga,kazi zilizofanyika hadi sasa ni kufanya usanifu na upembuvu ambapo kazi ya ujenzi wa daraja hilo itafanywa kwa ushirikiano kati ya TANROADS Mkoa wa Ruvuma na Lindi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.