BAADHI ya wananchi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wamesema,miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,imewafanyia mambo makubwa na kuitendea haki wilaya hiyo kwa kutatua kero na changamoto nyingi zilizokuwepo tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961.
Wamesema,moja kati ya kero kubwa ilikuwa barabara za kuunganisha kijiji kimoja hadi kingine,lakini sasa kero hiyo haipo kufuatia serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura) kutoboa na kufanya matengenezo ya barabara nyingi wilayani Nyasa.
John Mkomola mkazi wa kijiji cha Ngumbo amesema, Rais serikali ya awamu ya sita imewatendea haki kwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo kuboresha barabara zilizorahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.
Mkomola ambaye ni Katibu wa CHADEMA kata ya Ngumbo wilayani humo,emeipongeza serikali kwa kazi kubwa iliyofanya ya kuimarisha na kuboresha barabara ambazo zimewezesha wananchi na vijiji vingi kufikiwa na huduma za kijamii.
Amesema,baadhi ya maeneo katika wilaya ya Nyasa hayakuweza kufikiwa na baadhi ya huduma za kijamii kwa kukosa barabara, hivyo kusababisha maisha yao kuwa magumu licha ya wilaya hiyo kuwa na rasimilia kubwa ya ardhi na ziwa Nyasa lenye samaki wengi.
Adolat Kapinga mkazi wa kijiji cha Lugali amesema,awali barabara ya Ngumbo-Litoho inayounganisha wilaya ya Nyasa na Mbinga haikuweza kupitika kwa urahisi kutokana na ubovu hasa mashimo mengi na makubwa katikati ya barabara na utelezi wakati wa kiangazi.
Hata hivyo ameeleza kuwa,katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia barabara hiyo imeimarika na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hizo mbili ambao sasa wanatembea kifua mbele na kufaidi matunda ya serikali yao.
Ameipongeza serikali kwa kuendelea kujenga na kuboresha barabara na kurudisha mawasiliano katika maeneo mengi ya wilaya hiyo ambayo hapo awali hayakufikika kwa urahisi kutokana na ubovu wa barabara.
“lazima tukubali tangu Rais Dkt Samia alipoingia madaraka miaka miwili sasa tunaona mabadiliko mengi na makubwa katika wilaya yetu,barabara hii haikuweza kupitika kirahisi, lakini sasa serikali kupitia Tarura imeiboresha na kuunganisha mawasiliano kati ya wilaya ya Mbinga na Nyasa”amesema Kapinga.
Kwa upande wake meneja wa TARURA wilaya ya Nyasa Thomas Kitusi amesema,barabara ya Ngumbo –Litoho yenye urefu wa km 6.59 ilitengewa jumla ya shilingi milioni 84 kwa ajili ya kufanya matengenezo kwa kiwango cha chanagarawe.
Aidha amesema,katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya barabara ikilinganisha na miaka ya nyuma.
Kitusi ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha nyingi zinazotokana na tozo na fedha za mfuko wa Jimbo ambazo zimewezesha Tarura kufanya matengenezo ya barabara nyingi za vijijini ambazo zimeleta mabadiliko makubwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.