SERIKALI kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,imeanza kazi ya kurejesha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua za masika katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Miongoni mwa barabara zilizoharibiwa na baadhi ya madaraja yake kusombwa na maji ni Barabara ya Mapera-Mikalanga -Ilela na Mitawa ambayo ilijifunga kutokana na kuharibika vibaya kwa kuwa na mashimo makubwa yaliyosababishwa na mvua za masika.
Meneja wa Tarura wilayani Mbinga Mhandisi Oscar Mussa amesema,serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 672 kurejesha tena miundombinu hiyo ili wananchi waweze kuendelea kuzitumia barabara hizo kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema,barabara hizo ziliharibika kutokana na mvua kubwa za masika zilizonyesha kuanzia mwezi Februari hadi mwezi Disemba mwaka jana, ambapo pia kalavati moja na madaraja manne yaliharibika na wameanza kuyajenga upya ili kurudisha mawasiliano katika maeneo hayo.
Alitaja gharama ya kurejesha upya miundombinu hiyo ni shilingi 672 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizo,na kuwaomba wananchi wawe wavumilivu wakati huu ambao serikali iko kazini.
Richard Milinga mkazi wa kijiji cha Ilela wilayani humo,ameishukuru serikali kwa kuanza kufanya matengenezo ya barabara hizo,kwani zilikuwa mbaya na kusababisha shughuli zao za kujiingizia kipato kusimama.
Milinga alisema baada ya kuharibika kwa barabara hizo,walikuwa kwenye wakati mgumu kwa kuwa hakuna usafiri wowote wa chombo cha moto iliyofika katika maeneo yao,badala yake walilazimika kutembea kwa miguu kutoka Ilela kwenda maeneo mengine kufuata huduma za kijamii.
Ameipongeza wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura)kwa kuchukua hatua za haraka kuanza matengenezo ya barabara hizo ambazo ni nguzo kuu ya kiuchumi.
Alisema,ukarabati huo utakapokamilika utawawezesha kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali zilizosimama takribani mwaka mmoja tangu miundombinu ya barabara ilipoharibika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.