Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma umeendelea na juhudi za kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda misitu ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.
Meneja wa TFS Wilaya ya Songea, Mhifadhi Issa Mlela, amewataka wananchi kushirikiana na serikali kudhibiti ukataji miti holela, ambao unaweza kusababisha ukame na kuathiri kilimo cha chakula na biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mlela amesema kuwa misitu ni rasilimali muhimu kwa kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, hivyo uharibifu wake unasababisha madhara makubwa kwa jamii.
Ameeleza kuwa TFS inatumia vyombo vya habari na mikutano ya kijamii kutoa elimu juu ya athari za uharibifu wa misitu na umuhimu wa kuilinda.
Katika juhudi za kulinda misitu, TFS imeimarisha utekelezaji wa sheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kudhibiti ukataji miti holela, uchomaji moto, na uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi. Aidha, kampeni za upandaji miti zimefanikiwa kupanda miti milioni 1.5 katika Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kurejesha uoto wa asili na kuimarisha mifumo ya ekolojia.
Mlela ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda misitu kwa kuepuka uharibifu wa mazingira, ili kuhakikisha rasilimali hii inabaki kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.