Kikao muhimu cha kujadili mikakati ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox kimefanyika wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma kikiwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa afya, na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.
Kikao hicho kililenga kuhakikisha wilaya inakuwa tayari kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utaripotiwa katika eneo hilo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru, Ndugu Milongo Sanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Simon Chacha, aliwataka wananchi kutohofia ugonjwa wa Mpox kwani hadi sasa hakuna mgonjwa aliyeripotiwa wilayani humo.
Alihimiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na kuchukua tahadhari zinazostahili ili kuzuia maambukizi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Bi. Grace Mhagama, aliwataka washiriki wa kikao hicho kuwa mabalozi wa afya kwa jamii, akisisitiza kuwa kila mtu ana jukumu la kueneza elimu kuhusu dalili, njia za maambukizi, na namna ya kujikinga na Mpox.
Alibainisha kuwa uelewa wa jamii utasaidia kudhibiti ugonjwa huo mapema.
Mganga Mfawidhi wa Wilaya hiyo Dr.Athumani Mkonoumo, aliwaeleza washiriki kuwa Mpox hauna tiba ya moja kwa moja, lakini wagonjwa hupatiwa matibabu ya kupunguza dalili.
Alielezea umuhimu wa utengaji wa wagonjwa ili kuzuia maambukizi zaidi na kusisitiza kuwa ufuatiliaji wa karibu wa visa vyovyote vinavyoshukiwa ni muhimu.
Afisa Afya wa Wilaya, Bwana Ayubu Majumbewima, alielezea hatua zinazochukuliwa na halmashauri katika kuelimisha jamii kuhusu Mpox
Alisema kampeni za uhamasishaji zinaendelea kupitia kliniki, mashule, mikutano ya hadhara, na vyombo vya habari na kwamba hospitali ya wilaya imetenga jengo maalum kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaobainika na ugonjwa huo, huku usafiri wa dharura ukiwa tayari kwa ajili ya wagonjwa na wataalamu wa afya.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.