Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wadau wa uchaguzi mkoani Ruvuma kutumia nafasi zao katika jamii kuwafikishia wanaruvuma taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Stanslaus Mwita, wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele kwenye mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea mkoani Ruvuma.
"Kufanikiwa kwa zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mkoa wa Ruvuma, kunategemea sana ushiriki wenu katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kandikishwa au kuhamisha au kuboresha taarifa zao," alisema Mwita.
Amebainisha kuwa katika mkoa wa Ruvuma zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku 7 kuanzia Januari 12 hadi 18, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea ambapo vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni.
Katika hatua nyingine Mwita amewakumbusha wadau na wananchi kuwa kadi zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika katika chaguzi zijazo, hivyo zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari halitawahusu wapiga kura wenye kadi hizo, na ambao kadi zao hazijaharibika, kupotea au hawajahama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine au taarifa zao hazijakosewa au hawahitaji kuboresha taarifa zao.
Naye Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Ruvuma, Salum Kateula, amesema mkoa wa Ruvuma utakuwa na awamu mbili za Uandikishaji ambapo awamu ya kwanza itahusisha halmashauri tano ikiwemo Songea MC, Songea DC, Mbinga DC, Mbinga TC na Nyasa DC ambapo uboreshaji huo wa Daftari utaanza Januari 12 hadi 18, 2025, na awamu ya pili itajumuisha Halmashauri tatu ambazo ni Namtumbo DC, Tunduru DC na Madaba DC ambapo zoezi hilo litaanza Januari 28 hadi Februari 3.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni zoezi muhimu linalofanyika ili kuhakikisha taarifa za wapiga kura ziko sahihi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025, kauli mbiu ya zoezi hili ni "Kujiandikisha Kupiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora."
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.