WADAU wa Elimu Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamempongeza Mwalimu Fidea Mapunda wa shule ya msingi Pambazuko kutokana na ubunifu wake wa kufundisha wanafunzi kupitia mapambo.
Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao katika hafla fupi ya kutambulisha mradi unaojulikana kama Elimu ya watoto nyumbani uliobuniwa na Mwalimu huyo.Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Heritage Cottage mjini Songea na kushirikisha baadhi ya walimu,waratibu Elimu Kata na wanafunzi wa shule za msingi.
Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Meya wa Manispaa ya Songea Jeremia Kilembe amesema kuwa Mwalimu huyo anastahili pongezi kutokana na ubunifu wake wa kufundisha wanafunzi kwa njia ya mapambo kwa kutumia vitambaa vya kwenye makochi vilivyofumwa kwa mchoro wa ramani ya Afrika,Tanzania na alama za Bendera ya taifa.
Kilembe amesema kuwa ubunifu uliofanywa na Mwalimu Fidea utasaidia kuwajengea uwezo watoto na wanafunzi wa kufahamu vitu wakiwa nyumbani badala ya kusubiri mpaka wanapokwenda kuanza shule ya chekechea na msingi.
Mmoja wa mwanafunzi wa shule ya Msingi Taifa Foundation mjini Songea Gloria Swila amesema kuwa kutokana na ubunifu wa Mwalimu huyo,umeweza kumjengea uwezo wa kuwajua wanyama wakali,wapole,alama ya Bendera ya Taifa,ramani ya Afrika na Tanzania kupitia mapambo.
“Nawaomba wazazi na walezi kuwatengenezea mazingira ya kielimu nyumbani watoto wao kwa kuwaandalia mapambo yanayoonesha wanyama wakali,wanyama rafiki,mapambo yenye rangi ya Bendera ya Taifa na vifaa vinavyotengenezwa kutokana na rasilimali ya miti’’,alisisitiza Gloria.
Naye Kaimu Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Songea Gerald Chavallah amempongeza Mwalimu Fidea kwa ubunifu wake na kuwataka walimu wengine kuiga mfano huo ili ujuzi huo uweze kutumika katika kuwafundisha watoto na wanafunzi wa shule mbalimbali katika manispaa ya Songea.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo Mwalimu Fidea Mapunda amelitaja lengo la kuanzisha mradi huo kuwa ni kwa ajili ya kumuandaa mtoto kupata elimu kupitia mapambo akiwa nyumbani.
“katika kukabiliana na Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia mtoto anapaswa kuwekewa mazingira wezeshi ya kujifunzia kupitia mapambo ya ndani kwa kufuma vitambaa vyenye picha ya wanyama wakali,wanyama rafiki,rangi za Bendera ya taifa,ramani ya Tanzania,ramani ya Afrika na kutengeneza vitu vinavyotokana na rasilimali za mit’’,alisisitiza.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 10,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.