vivutio vya mambokale vinapaswa kupewa kipaumbele kwa sababu vinachangia katika kukuza historia na kuendeleza utalii.Wilaya ya Nyasa imebarikiwa pia na utalii wa mambokale ambao unavutia wengi kujua masuala mbalimbali ya kihistoria katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Vivutio vya mambokale katika wilaya ya Nyasa vimegawanyika katika sehemu ambazo ni historia za mambokale zilizofanywa na viongozi wa nchi katika maeneo mbalimbali na kuingia kwa dini na madhehebu ambayo yameacha alama kubwa.
Baadhi ya vivutio vya mambokale katika wilaya ya Nyasa ni kile kilichopo Katika eneo la Mbamba bay ambapo Rais Mstaafu wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Oscar Kambona katika harakati za kudai Uhuru walilala hapo miaka ya 1956 nyumbani kwa dada wa Oscar Kambona ambapo palikuwa na ofisi ya chama cha TANU.
Magavana wa Shirikisho wa Rodesia na Nyasaland walikutana katika (Rest House) eneo la Mbamba bay jengo ambalo kwa sasa ni ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbambabay wakiwa na lengo la kuagana kutokana na vuguvugu la waafrika kudai Uhuru 1959 kushika kasi. Jengo hilo lilijengwa kwa miti.
Kivutio kingine cha utalii wa mambokale ni Kuingia kwa dini na madhehebu mbalimbali pia sehemu kubwa ya utalii wa nyasa unaobeba historia.
Mwaka 1981 wananchi wa Lituhi waliahamishwa kwa ajili ya kupisha mafuriko yaliyosababishwa na kufungwa kwa Mto Shire nchini Malawi na baadaye mwaka 1987 Mwalimu Nyerere akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi alifika kwa ajili ya kutoa maamuzi magumu ya kuwarudisha katika makazi yao ya awali na baada ya kuongea na wananchi hao kwenye mti mtebhele (muyombo) ambao upo katika kijiji cha Mwera mpya kata ya Lituhi na baadae alipiga picha na mkewe katika eneo hilo kabla ya kuondoka.
Dini iliyoanza kuingia katika wilaya ya Nyasa ni dini ya Kikristo,Mwinjilisti wa kwanza wa Anglikana William Parcival Johnson alianza kuhubiri Februari 9,1881 na akahamia rasmi Liuli mwaka 1906, alifariki Oktoba 11,1928 na kuzikwa Liuli.
Wakati huo ilitambulika kwa jina la DayosisI ya Nyasaland, ikafuata Dayosisi ya Southwest Tanganyika mwaka 1952 na baadaye kuitwa Dayosisi ya Ruvuma mwaka 1971.
Mwinjilisti William Parcival Johnson awali wakati anaingia Nyasa alikuwa na lengo la kujenga kanisa Kijiji cha Hongi ambapo wenyeji hawakutaka na alifukuzwa ndipo akakilaani kijiji cha Hongi kiwe na sisimizi wengi, pia kiote majani yaitwayo mapelele ambayo kabla yake hayakuwapo. Historia na simulizi za wahenga zinatoa simulizi hizo za kusisimua.
Historia inaonesha kuwa Kanisa Katoliki wilayani Nyasa liliingia mwaka 1912 huko Nkaya na kuanzisha Parokia na baadae kujenga kanisa kubwa la Lituhi mwaka 1939. Mwanzilishi akiwa ni Padre Henrich Kunster.
Uislamu uliingia Nyasa mnamo mwaka 1928, Sheikh wa kwanza aliitwa Mzee Bin Amanzi, Ilipofika mwaka 1932 Waasisi walijenga msikiti ambao miongoni mwao ni Twaib Abdallah, Akida Wabu, Mdoka, Ajali Hassan, Mfaume Bolin na Issa Kimambe.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.