Sekretariati ya Mkoa wa Ruvuma Kufanya Ufuatiaji Shirikishi wa Ukusanyaji Mapato ya Ndani kwenye Halmashauri
Katibu Tawala wa Ruvuma Prof.Riziki Shemdoe ameagiza kufanyika ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye mamlaka zote za serikali ya mitaa .
Ametoa agizo hilo hivi karibuni kufuatia ripoti za Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuonyesha mkoa wa Ruvuma umefanya vibaya katika ukusanyaji mapato ya ndani robo ya kwanza mwaka 2018/2019 .
“Kila mkuu wa idara na kitengo katika sekretariati ya mkoa huu anatakiwa atoke na kwenda kwenye halmashauri kufanya ufuatiliaji wa mapato katika vyanzo vilivyoanishwa katika idara yake na kutoa ushauri wa kuongeza kasi ya ukusanyaji”amesema Prof.Shemdoe.
Katibu Tawala Mkoa ameagiza kuwa timu ya ufuatiliaji ihoji namna halmashauri zinavyokusanya katika vyanzo vyote 53 vilivyoanishwa kwenye Sheria kisha watoe ushauri wa namna bora ya kufanikisha lengo .
Kwa mujibu wa taarifa ya robo mwaka Julai hadi Septemba 2018 iliyotolewa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Selemani Jaffo ilionyesha kuwa mkoa wa Ruvuma ulikuwa kati ya mikoa iliyofanya vibaya kwa ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika kutekeleza agizo ufuatiliaji wa ukusanyaji mapato ya ndani umeanza kwenye halmashauri za wilaya ya Mbinga,Mji Mbinga ,Madaba DC,Namtumbo DC,Songea DC na Nyasa DC kuona sababu zilizosababisha kufanya vibaya.
Akizungumza kwa niaba ya timu ya ufuatiliaji ya mkoa Mwanasheria toka Sekretariati ya mkoa Seligius Ngahi amesema ufuatiliaji huu utasaidia kutoa ushauri kwa viongozi wakuu wa mkoa na Halmashauri kujua kwa kina mapungufu yaliyopo kwenye zoezi la ukusanyaji mapato ya ndani na kuchukua hatua za kudhibiti.
Aidha,Mkurugenzi wa Mji Mbinga Grace Quintine ameshukuru uamuzi wa Mkoa kuunda timu ya ufuatiliaji ili isaidie wataalam wa Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji pia kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
“Nashukuru nimepata uelewa kuhusu suala la mapato kwenye sekta ya ardhi kwenye halmashauri yangu kuwa tunazo fursa za kuongeza mapato kwa kuuza viwanja na vibali vya ujenzi” alisema Quintine.
Timu ya ufuatiliaji mwenendo wa ukusanyaji mapato ya ndani kwenye halmashauri itakapokamilisha kazi ya kutembelea na kukagua halmashauri zote nane za mkoa itatoa taarifa kamili ya kilichobainika kufanya Ruvuma isifanye vizuri kwa Katibu Tawala Mkoa .
Mwisho
Songea
15 Januari,2019
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.