UGONJWA wa usubi umetajwa kuwa bado ni tishio kwa wananchi mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele mkoani Ruvuma, Dr.Charles Hinju kwenye mafunzo ya kudhibiti na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika jamii kwa wajumbe wa RHMT.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,mjini Songea,Dr.Hinju ameitaja Wilaya ya Nyasa kuwa inaoongoza kwa maambukizi ya ugonjwa wa usubi kwa asilimia 18.
“Katika zoezi la utafiti la kuchukua damu kwa Watoto wadogo kuanzia miaka mitano Kwenda tisa,lilionesha kuwa katika Mkoa wa Ruvuma asilimia 4.2 walikuwa na ugonjwa wa usubi,wilaya ya Nyasa pekee ilionekana ina maambukizi makubwa ya asilimia 18.33’’,alisisitiza Dr.Hinju.
Kutokana na tishio la maambukizi ya ugonjwa wa usubi,Mkoa mwezi huu Agosti umedhamiria kutoa dawa za kinga tiba ya magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele katika jamii katika wilaya zote.
Hata hivyo amesema kwa mwaka huu kipaumbele kitakuwa zaidi kwa ugonjwa wa usubi ambapo viongozi ngazi ya wilaya na Mkoa wataandaliwa Pamoja na kuhamasisha jamii ili kufahamu zoezi zima la ugawaji dawa kinga kwa jamii litakavyofanyika.
Amesisitiza kuwa dawa kinga hizo zitatolewa kwa wananchi wote ambao wanapaswa kunywa dawa wenye umri wa kuanza miaka mitano na kwamba dawa hizo hazitatolewa kwa akinamama wajawazito na wagonjwa wenye magonjwa waliolazwa ambao hawahitajiki kunywa dawa hizo.
Amesema asilimia 80 ya jamii inahitajika kupata dawa kinga hizo ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa usubi ambao amesema unaleta athari kwenye Ngozi,macho na kuhusisha ugonjwa wa kifafa.
Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha kuwa wanakunywa dawa kinga hizo ili kukabiliana na usubi kwa sababu ugonjwa wa usubi katika Mkoa wa Ruvuma ni changamoto kubwa.
Kwa mujibu wa Dr.Hinju,utafiti uliofanyika mwaka 1997 ulionesha kuwa asilimia 40 hadi 71 waligundulika kuwa maambukizi ya ugonjwa wa usubi mkoani Ruvuma.
Utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2011 mkoani Ruvuma kuhusiana na ugonjwa wa usubi ,ilibainika kuwa asilimia 4 walikuwa na usubi na kwamba hali ilikuwa mbaya zaidi katika wilaya ya Nyasa iliobainika kuwa na maambukizi makubwa.
Dalili za ugonjwa wa usubi ni Mgonjwa kupata viupele upele kwenye ngozi yake ya mwili,Mgonjwa kupatwa na shida ya upofu wa macho,Mgonjwa kupatwa na miwasho ya mara kwa mara kwenye ngozi yake ya mwili,Joto la mwili kuwa juu au mgonjwa kuwa na homa,Mgonjwa kukosa hamu ya kua chakula na Ngozi ya mwili kuchuchuka
Wizara ya Afya imedhamiria kuendeleza juhudi za kumezesha kinga tiba pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa usubi ili kufikia lengo la mwaka 2030 ugonjwa huo uweze kutokomezwa.
Ugonjwa wa usubi unaathiri ngozi ya binadamu, kupatwa na homa kali, kutokwa na vipele mwilini, kuhisi uwasho mkali pia unaweza kusababisha upofu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya,ugonjwa wa usubi umeenea katika Halmashauri 29 ambapo takribani asilimia 7.02 ya watu wapo katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu nchini. Magonjwa mengine ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele na yanadhibitiwa kwa ugawaji dawa ni matende, trakoma, kichocho,minyoo ya tumbo na usubi.
Mikoa mingine nchini inayokabiliwa na ugonjwa wa usubi ni Tukuyu mkoani Mbeya ,Mahenge mkoani Morogoro na Mkoa wa Tanga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.