Katika juhudi za kuboresha elimu ya juu nchini Tanzania, ndoto ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mkoa unakuwa na chuo kikuu inaendelea kutekelezwa kwa vitendo.
Mkoa wa Ruvuma sasa utajivunia kuwa mwenyeji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa tawi la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika Manispaa ya Songea.
Kwa mujibu wa Meneja wa Chuo cha Uhasibu Arusha Kampasi ya Songea, Dkt. Bakari Mashaka, ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 18.5, fedha ambazo zimetolewa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Chuo hiki kipya kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 10,000 wa programu mbalimbali, jambo linaloashiria mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu na uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Safari ya Chuo cha Uhasibu Songea
Kwa sasa, IAA Kampasi ya Songea inatoa huduma zake katika jengo la TTCL, ghorofa ya pili, mjini Songea. Kozi zinazotolewa ni pamoja na Diploma ya Usimamizi wa Biashara, Uhasibu, TEHAMA, Fedha na Benki, pamoja na masomo ya ngazi ya uzamili katika fani za Biashara, Fedha, TEHAMA, Uongozi na Usimamizi wa Rasilimali.
Katika mahojiano maalum, Dkt. Mashaka alifafanua kuwa chuo hicho kinajikita katika kuwaandaa wanafunzi kwa ujuzi wa vitendo, hasa katika ujasiriamali ambapo amelitaja lengo kuu ni kuhakikisha wahitimu hawategemei tu ajira, bali wanakuwa wabunifu na wajasiriamali wa kujitegemea.
Fursa kwa Wananchi
Afisa Uhusiano wa IAA Kampasi ya Songea, Nuru Meshack, ameeleza kuwa baadhi ya wazazi huamini kuwa mwanafunzi aliyepata daraja la nne katika mtihani wa kidato cha nne hawezi kuendelea na masomo.
Hata hivyo anafafanua kuwa ufaulu wa daraja la nne (isipokuwa katika masomo ya dini) unaruhusu mwanafunzi kujiunga na chuo, hivyo akawahamasisha vijana kuchangamkia fursa zilizopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Mwaitete Cairo, ameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kutoa eneo la hekari 71 kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu hicho.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa chuo kikuu hicho utaanza mara moja kwa kutumia mfumo wa ‘force account’, hivyo wananchi wa Songea wanapaswa kujiandaa kupata nafasi za ajira na fursa za kibiashara zitakazotokana na mradi huu.
Mchango wa Ujenzi kwa Maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma
Eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki lipo katika kata ya Tanga, likizungukwa na maeneo muhimu ya kiuchumi kama vile Stendi Kuu ya Mabasi ya Tanga, Machinjio ya Kisasa na Hospitali ya Rufaa ya Manispaa ya Songea.
Hii inaashiria kuwa uwekezaji huu hautasaidia tu elimu, bali pia utachochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Songea na mkoa mzima wa Ruvuma.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano, amepongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kwa hatua hii muhimu, akisema kuwa wamejibu kilio cha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kutaka taasisi za elimu ya juu mkoani humo.
Kwa jumla, ujenzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha Kampasi ya Songea si tu utasaidia kuinua kiwango cha elimu, bali pia utafungua milango ya maendeleo na ajira kwa wakazi wa Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Wakati huo huo cha Uhasibu Arusha (IAA), kimejipanga kufanya maboresho Makubwa ili kwendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuanza kutumia madarasa mtandao ili kuwezesha kutoa elimu kwa kundi kubwa la wanafunzi maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi
Madarasa hayo ya kisasa yatamwezesha mwalimu atakayekuwa kwenye chumba cha darasa katika kampasi zake Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Babati mkoani Manyara na Songea na nchi watakazofungua matawi Sudan Kusini na Comorro kusoma kwa wakati mmoja.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.