Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), Mkoa wa Ruvuma umeonesha hatua kubwa za maendeleo katika kupunguza maambukizi na kuboresha huduma kwa waathirika.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa mwaka 2024, Ruvuma inakadiriwa kuwa na watu wanaoishi na VVU (WAVIU) 68,237. Kati yao, wanaume ni 24,959 (asilimia 37) huku wanawake wakiwa 43,238 (asilimia 63).
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Luois Chomboko anasema Watoto walio na umri chini ya miaka 15 ni 2,382 (asilimia 3.5), huku watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea wakifikia 65,855 (asilimia 96.5).
Kwa upande wa halmashauri, Manispaa ya Songea inaongoza kwa idadi kubwa ya WAVIU ikiwa na watu 18,398, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru yenye watu 9,888, na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ikiwa na watu 9,003.
Kupungua kwa Maambukizi Mapya ya VVU
Mojawapo ya mafanikio makubwa ya Mkoa wa Ruvuma ni kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU.
Idadi ya maambukizi mapya imeshuka kwa watu 279, sawa na asilimia 28.6, kutoka watu 2,168 mwaka 2023 hadi 1,889 mwaka 2024.
Wanawake wanaendelea kuathirika zaidi, wakihusisha asilimia 64.8 ya maambukizi yote (watu 1,225), huku vijana wa umri wa miaka 15-24 wakiwa na maambukizi 651 (asilimia 34).
Kwa watoto walio chini ya mwaka mmoja, maambukizi mapya yamefikia 168, sawa na asilimia 9.
Hatua Kubwa Katika Udhibiti wa VVU
Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kutekeleza afua mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya VVU, ikiwa ni pamoja na Kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 12.9, kutoka watu 3,168 mwaka 2022 hadi 1,889 mwaka 2024,WAVIU 57,421 (asilimia 84.1) wanajua hali zao za maambukizi,WAVIU 57,160 (asilimia 99.5) wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU na WAVIU 55,445 (asilimia 97.2) wamefanikiwa kufubaza VVU kwa kiwango kinachopunguza hatari ya maambukizi mapya.
Kupungua kwa Vifo na Unyanyapaa
Mafanikio mengine makubwa ni kupungua kwa idadi ya WAVIU waliopotea katika matibabu, kutoka watu 1,472 (asilimia 2.5) mwezi Aprili 2024 hadi 300 (asilimia 0.5) mwezi Desemba 2024.
Aidha, idadi ya vifo miongoni mwa WAVIU imepungua kutoka vifo 11 kwa kila watu 1,000 mwaka 2020 hadi kifo 1 kwa kila watu 1,000 mwaka 2024.
Kiwango cha unyanyapaa dhidi ya WAVIU pia kimepungua kutoka asilimia 64.5 mwaka 2012 hadi asilimia 25.5 mwaka 2024, hatua ambayo inatoa matumaini makubwa kwa jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.