Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo imebarikiwa kwa kuwa na neema ya vivutio lukuki na adimu vya utalii wa ikolojia na kiutamaduni.
Hifadhi ya Gesimasowa yenye ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 760 ambayo ipo katika Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea,ni miongoni mwa vivutio adimu vya utalii.
Hifadhi hiyo ilianzishwa kama msitu wa hifadhi mwaka 1975 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa zamani Hayati Dk.Lawrence Gama mwaka 1975.Hatimaye mwaka 2015,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kipindi hicho hayati Said Mwambungu alisimamia mchakato wa kupandisha hadhi msitu huo na kuwa hifadhi ya Taifa.
Moja ya vivutio vilivyopo katika hifadhi hii ni mapumziko ya ndege maarufu duniani wanazaliana katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo iliyopo Makete mkoani Njombe wanaitwa kitaalam Derhams wenye uwezo wa kuruka toka bara moja hadi bara jingine.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa ndege hao wanapumzika hapa kwa miezi kadhaa kisha wanaendelea na safari kupitia Bonde la ufa hadi ziwa Nyasa hatimaye wanasafiri hadi nchini Afrika ya Kusini na mabara mengine.
Kulingana na Challe,hifadhi ya Gesimasowa ni mapito ya ndege hao ambao wanatoka Kaskazini mwa Afrika kuelekea Afrika ya Kusini ambao wanafuata milima ya Livingstone iliyopo ziwa Nyasa na kwamba ndege hao pia wanapumzika Mwambao mwa ziwa Nyasa hasa katika eneo la Kihagara ambapo kuna mazingira ambayo yanavutia ndege hao kuishi.
Kwa mujibu wa Challe,Hifadhi ya Gesimasowa pia ina mfumo wa ikolojia wa pori la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa sababu ni mapitio ya wanyamapori wanaotoka katika Pori la Akiba la Selous wanapita kuelekea Bonde la ziwa Nyasa kupitia pori la Liparamba hadi Hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji ambapo wanyama wanakwenda nchini Msumbiji na kurudi Tanzania.
“Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Ruvuma kimeridhia hifadhi hii kupandishwa hadi kuwa Pori la Akiba la Gesimasowa,mchakato wa kutangaza rasmi katika gazeti la Serikali,Gesimasowa kuwa pori la Akiba upo katika hatua za mwisho’’,anasisitiza Challe.
Wanyama ambao unaweza kuwaona katika hifadhi ya Gesimasoa ni tembo, simba,ndege, nyati, pofu na samaki adimu duniani aina ya mbelele na mbasa.
Hifadhi hii pia ni maingiliano ya mito miwili ya Hanga na Lutukira ambayo inatengeneza mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa. Mto huo ndiyo mazalia ya samaki aina ya mbelele na mbasa ambao katika duniani nzima wanapatikana ziwa Nyasa pekee.
Imeandikwa na Albano Midelo,Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.