WATANZANIA wametakiwa kuiamini Serikali yao juu uwekezaji wa Bandari ya Dar es slaam uliofanywa na mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) na kampuni ya DP Word.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiuma wilayani Tunduru Daniel Malukuta,wakati wa mahafali ya 15 ya chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kiuma(KICoHAS) na mahafali ya tano tangu kuanza kwa ngazi ya stashahada na ya kwanza kwa ngazi ya stashahada ya mafunzo ya utabibu yaliyofanyika chuoni hapo.
Alisema serikali imefanya hivyo kwa nia njema kwa sababu uwekezaji huo kati ya Serikali na kampuni ya DP Word una manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi yetu,hivyo Watanzania tunapaswa kuunga mkono,badala ya kutumia muda mwingi kubeza mpango huo.
Alisema,hata pale wanapotaka kuikosoa Serikali ni vyema ikatumika busara na lugha rafiki badala ya kutanguliza kashifa na maneno ya kuhudhi yanayoweza kuwagawa Watanzania.
“sasa hivi hapa nchini habari kubwa inayoendelea ni juu ya uwekezaji wa Bandari yetu uliofanywa na Serikali,kumekuwa na upotoshaji mkubwa na bahati mbaya suala hili linaonekana kushabikiwa sana,nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kuiamini serikali na hata tunapokosoa basi tutumie lugha rafiki na watu wanaoelekezwa wanasikia na watalifanyia kazi”alisema Malukuta.
Alisema,kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Kiuma linapenda watu wake na jamii kwa ujumla kueleza shida na maoni yao kwa utaratibu na siyo kutumia lugha za kuhamasisha vurugu na maandamano ambayo hayana tija na afya na siyo utaratibu katika nchi yetu.
Malukuta ameishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa uliotoa kwa taasisi ya Kiuma hali iliyo wawezesha kutekeleza masuala mbalimbali ya kiroho na kuwapatia watanzania hasa vijana elimu na stadi mbalimbali ili ziweze kuwasaidia katika kukabiliana na maisha.
Amewataka wahitimu kwenda kuwa chachu ya kuharakisha kukua kwa uchumi,kutoa mchango kwa jamii,kuwa waaminifu na waadilifu kulingana na maadili ya taaluma zao na kuonyesha umahirikatika kazi zao ili kuwa mfano wa kuigwa utakao kiletea heshima chuo hicho na taasisi ya Kiuma.
Aidha,amewaasa wahitimu hao kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu vinavyokwenda kinyume na maadili na utamaduni wa nchi yetu ikiwemo tatizo la ushoga lililoanza kushamiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini na Ulimwenguni.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Mariana Njeama alisema, katika mahafali ya mwaka huu jumla ya wahitimu 130 wamehitimu fani mbalimbali kati yao wahitimu wa uuguzi na ukunga ngazi ya shahada wako 73 na utabibu wa ngazi ya stashahda wako 41.
Alisema,chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi-Kiuma hadi sasa kimefanikiwa kutoa wana chuo(wahitimu)takribani 243 kwa ngazi ya stashahada walioanza mwaka 2019 na wanaoendelea na mafunzo yao ni 335.
Alisema,kwa ujumla ufaulu wa wanachuo ni wa hali ya juu,kwani waliomaliza mwaka jana 2022 ufaulu wao ulikuwa asilimia 99.9 kwani kati yaw ana chuo 88 aliyeshindwa kufaulu ni mmoja.
Wahitimu hao katika risala yao iliyosomwa na Sarafina Kilagwa walisema,walianza mafunzo yao mwaka 2020 katika kada ya utabibu,uuguzi na ukunga wakiwa jumla ya wana chuo 149 kati yao kada ya uuguzi na ukunga 81 na utabibu 69.Alisema,katika mafunzo yao ya miaka mitatu wamefanikiwa kuimarisha taaluma ya chuo, kwa kupata matokeo chanya katika mitihani hususani ile ya wizara,chuo kupata maabra ya kisasa yenye vifaa vyote na kurahisisha kujifunza kwa vitendo zaidi kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.