VIONGOZI wa Dini na Serikali mkoani Ruvuma,wameipongeza taasisi ya MNAK Investment yenye makao yake makuu mjini Songea kwa ubunifu wake wa kuanzisha mradi wa kusaidia mavazi watu wenye uhitaji wakiwemo mahabusu na kuwapatia mitaji warekebishwa ambao wamemaliza vifungo vyao magereza kupitia kilimo.
Pongezi hizo zilitolewa jana na viongozi hao wakati walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa huduma ya MNAK kwa warekebishwa waliomaliza vifungo vyao magereza uliofanyika kwenye bustani ya manispaa ya Songea mkoani humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,Afisa tarafa Songea mjini na mashariki Dismas komba amepongeza ndoto za mkurugenzi wa taasisi hiyo mwalimu Neema Kajange kwa madai kuwa ubunifu wake utasaidia kuwajengea uwezo kimaendeleo na kuwainua kiuchumi walengwa hao.
Komba amewataka wadau wengine mbalimbali kujitokeza katika kuunga mkono huduma hiyo kwa ajili ya kusaidia walengwa hao mavazi,vitendea kazi,mitaji na kuacha tabia ya kuwanyanyapaa pindi wanaporudi uraiani baada ya kumaliza vifungo vyao magereza.
Naye mkuu wa gereza la mahabusu Songea Juma Mgumba ameipongeza taasisi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kusaidia mavazi,viherehani,sabuni,fedha,mafuta na kuwasaidia mitaji ambapo ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwatenga watu hao kwa madai kwamba baadhi yao wanapomaliza vifungo vyao wanakuwa watu wema na wenye ujuzi mbalimbali ikiwemo ujenzi,ufugaji,ushonaji na kilimo.
Nao viongozi wa Dini wakizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi huo wameipongeza taasisi hiyo kwa kusaidia mahabusu na warekebishwa misaada mbalimbali pindi wanapomaliza vifungo vyao kwa madai kwamba kitendo hicho ni cha Kimungu ambapo wameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na changamoto ya uchomaji moto wahalifu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa taasisi ya MNAK Investment Neema Kajange alisema kuwa lengo kubwa la taasisi yake ni kuwapatia mitaji warekebishwa kupitia kilimo ambapo amedai kuwa mpaka sasa taasisi hiyo imefanikiwa kuwawezesha na kufanya nao kazi warekebishwa watatu ambapo mmoja ni fundi kushona,wa pili fundi ujenzi na mwingine ni mkulima.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.