Na Albano Midelo
Katika pembe ya kusini mwa Tanzania,Ziwa Nyasa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma kuna hazina ya asili ambayo bado haijagunduliwa na wengi .
Visiwa vitatu vya Mbambabay, Lundo na Puulu,hivi si visiwa vya kawaida; ni visiwa vyenye hadithi, historia na mandhari ya kuvutia kiasi cha kuibua hisia na hamu ya kutaka kufahamu zaidi.
Mbambabay: Kisiwa cha Mapango na Samaki wa Mapambo
Kisiwa cha Mbambabay, kinachotajwa kuwa moja ya vivutio vya utalii wa kipekee, kimejaa mapango yanayotumika na wavuvi kama hifadhi salama wakati wa dhoruba kali.
Ni mahali pa asili ambapo mazingira yanazungumza ,hewa safi, sauti za ndege, na mwonekano wa samaki wa mapambo wanaoangaza chini ya maji safi ya Ziwa Nyasa.
Kwa wapenzi wa mazingira ya kuvutia na utulivu, kisiwa cha Mbambabay ni patanisho na sehemu asili inayovutia wengi.
Lundo: Historia Yenye Machungu na Mafundisho
Kisiwa cha Lundo kinabeba simulizi ya binadamu na jamii ,historia ya wagonjwa wa ukoma waliotengwa na kupelekwa kuishi kisiwani humo wakati wa utawala wa wajerumani
Makaburi ya waliopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huo bado yapo, yakielezea namna jamii ya wakati huo ilivyokabiliana na hofu ya maradhi.
Waliopoteza maisha walizikwa kwa kufunikwa na tope, imani ikisema hilo lingesaidia kutokomeza ugonjwa wa ukoma.
Lundo si tu kivutio cha kiasili, bali pia mahali pa kutafakari kuhusu historia, utu na maendeleo ya kijamii.
Puulu: Makazi ya Ndege wa Ajabu
Kisiwa cha Puulu, kilichopo Kata ya Liuli, ni mahali panapopaswa kutembelewa na kila mpenda maajabu ya asili.
Kisiwa hiki Kina mazalia ya samaki wa aina nyingi, wakiwemo wale wa mapambo. Lakini kivutio cha kipekee zaidi ni ndege maarufu duniani ajulikanaye kama ngwazi, anayejulikana kwa ustadi wake wa kipekee wa kuvua samaki kutoka majini.
Visiwa hivi ni hazina ambayo inahitaji kuangaziwa zaidi, kutangazwa kitaifa na kimataifa, na kuwekewa miundombinu rafiki ili kuwavutia watalii wa ndani na wa kimataifa.
Wilaya ya Nyasa, kupitia vivutio hivi, inaweza kuwa kitovu kipya cha utalii endelevu kusini mwa Tanzania .
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.