Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ametahadharisha vitendo vya uharibifu wa mazingira vinageuza mazingira ya Mkoa na kupoteza uoto wake wa asili na kusababisha ukame na jangwa.
Kanali Abbas ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza katika maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea.
Amesema kutokana na ongezeko la watu katika Mkoa na Taifa kwa ujumla,watu wengi wanatumia nishati ya kuni,mkaa na mbao kwa matumizi mbalimbali hali ambayo inachochea kuongezeka kwa kasi ya uvunaji wa mazao ya misitu,kilimo cha kuhamahama na uchomaji moto misitu.
“Hali hii husababisha kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi kama kuongezeka kwa joto katika uso wa nchi na kubadilika kwa kalenda na upatikanaji wa mvua,hivyo tusipobadilisha vitendo vyetu vya ukataji miti na uchomaji wa mkaa,tutageuza mazingira ya Mkoa wa Ruvuma kupoteza uoto wake wa asili’’,alisisitiza.
Hata hivyo Kanali Abbas amezihimiza Taasisi za serikali na binafsi ,vikundi vya vijana na akinamama kupanda miti kwa wingi ,kutumia nishati mbadala kama vile mabaki ya mazao ya misitu,gesi,majiko sanifu,kuchoma tofali kwa kutumia pumba za mpunga badala ya kutumia kuni.
Ameziagiza Halmashauri zote mkoani Ruvuma kusimamia kikamilifu sera,sheria ndogo na miongozo mbalimbali ya utunzaji wa mazingira na matumizi mazuri ya raslimali kwa kuhakikisha wanakuwa na vitalu vya miche ya miti na kupanda miti katika maeneo yaliyoathiriwa.
Kanali Abbas ameagiza pia kulinda vyanzo vya maji,kudhibiti uchomaji moto holela kwenye msitu na kuwawezesha wananchi kupata miche mbalimbali ya miti ya matunda,maua na miti kwa ajili ya mbao ili kukuza uchumi na kuhifadhi mazingira.
Amewaasa wananchi wazingatie umbali wa kulima toka kwenye vyanzo vya maji ambao ni mita 200 kwenye chemchem na mita 60 kwenye mito na kudhibiti kilimo cha kuhamahama ambacho hakina tija kwa kuwa kinajihusisha na uchomaji moto na ukataji wa miti.
Amekitaja chanzo kingine cha uharibufu wa mazingira ni kupitia ufugaji holela na usafirishaji wa mifugo nje ya njia zilizowekwa ambapo ameagiza kudhibiti ufugaji usiozingatia taratibu na kuhakikisha wafugaji wanafuga kulingana na ukubwa wa eneo.
Mkuu wa Mkoa pia amewaagiza watendaji kuweka mifumo mizuri ya ukusanyaji taka katika miji na mitaa sanjari ya kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo kwa kiwango kikubwa inasababisha uharibifu wa mazingira hasa ardhini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amesema wananchi wa Manispaa ya Songea wameadhimisha siku ya mazingira kwa kufanya usafi katika eneo la hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ,eneo la Mwengemshindo ambako wamefanya usafi eneo la hekari nne na nusu kati ya hekari tano zinazotakiwa kufanyiwa usafi.
Amesema wanatarajia wiki hii kukamilisha kufanya usafi katika eneo hilo Pamoja na kupanda miti ya matunda ambapo amesema Rais Samia ametoa mabilioni kwa ajili ya miundombinu na vifaa tiba vya hospitali hiyo.
Kila mwaka Juni 5 huadhimishwa siku ya mazingira Duniani ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika na ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame.
Vijana wahamasishaji wakiadhimisha siku ya mazingira Duniani ,maadhimisho ambayo kimkoa yamefanyika Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.